Na Khadija Kalili   , Michuzi TV 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani aanza ziara ya kikazi, asisitiza ubunifu katika miradi ya maendeleo

Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, leo ameanza ziara yake ya kikazi katika Halmashauri za Mkoa wa Pwani kwa kutembelea Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Katika ziara hiyo, Mnyema amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuongeza mapato ya Halmashauri pamoja na Mkoa kwa ujumla.

"Naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kubuni vyanzo vipya vya mapato. Hili ni miongoni mwa maagizo niliyopatiwa ili kusaidia kuongeza mapato ya Mkoa wetu," alisema Mnyema.

Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa kuendelea kubuni na kusimamia miradi mbalimbali yenye tija, ambayo imesababisha ongezeko la mapato ya Manispaa hiyo kila mwaka.

Mnyema aliwataka watumishi wa Manispaa hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu, uadilifu, na bidii, ili kutoa huduma bora kwa wananchi. Alisisitiza pia umuhimu wa uwajibikaji na uaminifu katika usimamizi wa fedha za umma, ili kudhibiti upotevu wa rasilimali na kuongeza ufanisi katika miradi ya maendeleo.

Akiwa katika Manispaa ya Kibaha, Katibu Tawala huyo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza – Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu, pamoja na mradi wa maduka ya biashara ya Kibaha Shopping Mall.

Ziara hiyo inalenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kufanya vikao kazi na watumishi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani. Kesho,  Katibu Tawala anatarajiwa kuendelea na ziara hiyo kwa kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...