Na WILLIUM PAUL, SAME.
MKUU wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro Kasilda Mgeni, ameonya kuwa serikali haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria wananchi watakaobainika kuharibu miundombinu ya maji, kwani kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi.
Kasilda alitoa kauli hiyo leo wakati akimkabidhi cheti cha pongezi Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Same - Mwanga (SAMWASA), Mhandisi Rashid Shaban Mwinjuma, kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ambapo alisema kuwa utaratibu huo ni sehemu ya jitihada za ofisi yake za kuzipa motisha taasisi za serikali zinazofanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato.
Aidha, alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuongeza juhudi za watumishi na taasisi katika kuimarisha huduma kwa wananchi.
Kasilda pia aliwataka wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya miradi ya maji ya SAMWASA na kuhakikisha wanalipa Ankara za maji kwa wakati, ili kurahisisha upatikanaji endelevu wa huduma hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa SAMWASA, Mhandisi Rashid Shaban Mwinjuma, alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Same kwa kutambua kazi zinazofanywa na mamlaka hiyo huku akieleza kuwa cheti hicho ni chachu kwa taasisi na watumishi wa taasisi hiyo kuongeza ubunifu katika ukusanyaji wa mapato.
Hata hivyo, Mhandisi Rashid Mwinjuma ameahidi kuendelea kutoa huduma kwa karibu kwa wananchi wa Same na Mwanga, sambamba na kufanikisha utekelezaji wa malengo ya serikali katika sekta ya maji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...