NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV



Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya Tanzania, Taifa Stars, imeanza kwa kishindo michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2025, baada ya kuichapa Burkina Faso mabao 2-0 katika mchezo wa ufunguzi uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo ulitanguliwa na shamrashamra za sherehe za ufunguzi wa mashindano hayo ambayo kwa mwaka huu yanafanyika nchini Tanzania, ikishirikiana na mataifa jirani ya Kenya na Uganda kama wenyeji wa pamoja.
Taifa Stars ilipata bao la kwanza kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wake chipukizi, Abduli Sopu, aliyefunga kwa mkwaju wa penati kufuatia rafu aliyochezewa Clement Mzize ndani ya eneo la hatari la Burkina Faso.
Bao la pili lilipatikana kipindi cha pili kupitia kwa beki mahiri, Mohammed Hussein, ambaye alitumia vyema nafasi aliyoipata na kuzamisha mpira wavuni, na hivyo kuimarisha ushindi wa Stars mbele ya mashabiki walioufurika uwanjani.
Kwa ushindi huo, Tanzania inaongoza kundi B linalojumuisha timu kutoka Mauritania, Madagascar, Afrika ya Kati na Burkina Faso, na imejiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele kwenye mashindano hayo.
Michuano ya CHAN 2025 inahusisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani pekee na inatarajiwa kutoa burudani ya aina yake kwa mashabiki wa soka barani Afrika, huku Tanzania ikiweka matumaini makubwa kwa kikosi chake kupata mafanikio makubwa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...