Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Mamlaka ya Afya ya Mimea na
Viuatilifu Tanzania (TPHPA) yazindua kifaa maalumu cha kisasa aina ya MinION cha kutambua vinasaba (DNA) za
mimea, Wadudu na magonjwa ambacho kinauwezo wa kufanya uchunguzi na kutoa majibu
papo hapo shambani ndani ya muda mfupi na hivyo kusaidia jitihada za serikali
za kutatua changamoto visumbufu vya mazao ya wakulima na kuongeza uzalishaji.
Akizungumza na Waandishi wa
habari, wadau wa kilimo na wananchi wengine kwenye banda la TPHPA ndani ya
viwanja vya maonesho ya kilimo nanenane kitaifa jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu
wa TPHPA Prof. Joseph Ndunguru amesema kuwa kupatikana na kifaa hicho ni
mkombozi katika utatuzi wa ya changamoto ya visumbufu vya mimea kwa wakulima
nchini.
“Kifaa hiki kilibuniwa nchini
Uingereza kwa lengo la kutambua virusi vya Zika na Ebora lakini sisi tumeweza kufanya
majaribio ya kina na kisha kuthibitisha kwa asilimoa 100% kuwa kinauwezo mkubwa
wa kutumika kwenye sekta ya kilimo na hivyo kuifanya Tanzania kuwa wa nchi ya kwanza
kuitumia teknolojia hii kutambua vinasaba vya wadudu, mimea lakini pia utambuzi
wa magonjwa kwa haraka mnoo” alibainisha Prof. Ndunguru.
Mkurugenzi huyo amesema kupitia
ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la chakula Duniani (FAO) na
Serikali ya Tanzania kupitia (TPHPA) wameweza kufanikiwa kupata vifaa hivyo 20
ambavyo vitakwenda kuwekwa kwenye vituo vya Mamlaka hiyo kwenye kanda zote na kushirikiana na wataalamu
wengne wa kilimo kubaini vinasaba mbalimbali vya wadudu na magonjwa sugu na ya mlipuko
kwenye maeneo yote ya Tanzania.
Aidha amebainisha kuwa kwa
kutumia kifaa hicho sasa Tanzania itaweza kuzalisha vyakula na bidhaa
zinazokidhi mahitaji ya masoko ya kimataifa kwakuwa watakuwa na uwezo wa kupima
na kuthibitisha ubora wa mazao kama yamekidhi viwango lakini pia kuzuia
uingizwaji wa mazao hasa vyakula ambavyo vina zuio kutokana na kuwa na vidudu
au magonjwa hatari kwa usala wa chakula na kilimo nchini.
“Teknolojia hii sio kwamba
tutaitumia sisi kwenye kilimo tuu la hasha, bali tunaweza kushirikiana na
wenzetu kwenye Wizara na Taasisi mbalimbali kwenye kutambua vinasaba na
majonjwa kama vile katika masuala ya uhifadhi kwenye kutambua mimea, viumbe
maji, lakini hata kwa wanyamapori na magonjwa ya binadamu inaweza kutoa majibu
haraka sana kuliko teknolojia tulizonazo sasa” alieleza Prof. Ndunguru.
Aliongeza “Tanzania tunajivunia
kuwa wa kwanza kutumia teknolojia hii na ni kutokana na jitihada kubwa
zinazofanywa na serikali yetu ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya kuhakikisha changamoto za visumbufu vya mazao vinabainishwa na
kukabiliwa kwa kutumia viuatilifu sahihi badala ya kubahatisha na kumuacha
mkulima akilia na kupoteza mazao yake”.
Awali Mkurugenzi wa Kurugenzi ya
afya ya mimea kutoka TPHPA Dkt. Benignus Ngowi amebainisha kuwa zipo changamoto
nyingi ambazo zinawatesa wakulima hususani magonjwa na wadudu na nyakati
nyingine yanapotokea magonjwa ya mlipuko huchukua muda mrefu kupata majibu toka
sampuli zinapochukuliwa na kupelekwa maabara lakini kwa kifaa hicho sasa
wanauwezo wa kupata majibu hapohapo shambani ndani ya dakika ishirini na kutambua
tiba yake.
Dkt. Ngowi amesema kumekuwa na
vilio kwa wakulima wa Nyanya, Migomba, Mihogo, Mahindi na mazao mengine ya
bustani na hiyo imekuwa ikitokana na wakulima kutumia viuatilifu kwa
kubahatisha bahatisha lakini kupitia kifaa hicho sasa hakutakuwa na kubahatisha
katika kukabili magonjwa na wadudu visumbufu.
“ Ukienda kwa wakulima wa mbogamboga
na matunda mfano nyanya utakutana na kilio cha mdudu hatari tuta ablsoluta wakulima wanamuita “Kantangaze”,
lakini pia kuna wadudu wengine kwenye matunda kama vile Nzi weupe “White flies”,
ukienda kwenye mihogo kuna magonjwa ya Batobato na michirizi ya kawahawia
ambayo inasambabishwa na wadudu hao lakini mkulima akiwaangalia anaweza kuona
wanafanana au ni mdudu wa aina moja lakini kuna aina nyingi za wadudu hao ambao
wanadhibitiwa kwa aina tofauti na sio dawa moja kama wakulima wanavyodhani na
mwisho wa siku hulalamika wametumia dawa na wadudu bado wanashambulia lakini
sasa kifaa hiki ni mkombozi” alifafanua Dkt. Ngowi.
Baada ya maonesho hayo tayari
timu ya wataalamu kutoka TPHPA wanatarajia kuweka kambi kwenye Halmashauri ya
wilaya ya Kilolo kwaajili ya kubaini changamoto za magonjwa na wadudu
wanasababisha hasara kwa wakulima wa mazao ya mbogamboga katika eneo hilo
maarufu kwa mazao hayo.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA UZINDUZI WA TEKNOLOJIA HIYO.
![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru akielezea Waandishi wa habari na wadau wa kilimo namna teknolojia hiyo inavyofanya kazi na faida yake kwa taifa. |
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...