Dar es Salaam, Agosti 17, 2025 – TPDC Runners Club leo imeungana na maelfu ya wakimbiaji kushiriki mbio kubwa za CRDB Marathon zilizofanyika katika Viwanja vya Farasi, Masaki, jijini Dar es Salaam. Mbio hizo zimehusisha umbali wa KM 5, KM 10, KM 21 na KM 42 na kuvutia washiriki kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Katika mbio hizo, TPDC Runners Club imepeperusha vyema bendera ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), baada ya wanachama wake kujitokeza kwa wingi kushiriki kwa ari kubwa. Ushiriki wa klabu hiyo umeendelea kuwa sehemu ya utamaduni wa wafanyakazi wa TPDC wa kufanya mazoezi ya pamoja, kushiriki mashindano mbalimbali ya michezo na kuendeleza falsafa ya kujenga afya bora, mshikamano wa kikazi na kutangaza Shirika.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mbio hizo, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC, Bi. Marie Msellemu, alisema:

“Ushiriki wetu kwenye CRDB Marathon unadhihirisha dhamira ya TPDC ya kuunga mkono michezo na kuhamasisha afya bora kwa wafanyakazi wake. Pia ni fursa muhimu ya kutangaza Shirika kwa umma kupitia matukio ya kijamii. Tunajivunia kuwa sehemu ya tukio hili kubwa ambalo linawaleta pamoja watanzania na taasisi”

Msellemu aliongeza kuwa klabu hiyo itaendelea kushiriki mbio na michezo mingine kadri inavyojitokeza, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano wa wafanyakazi na pia mchango wa TPDC katika kukuza michezo nchini.

Kwa upande wao, waandaaji wa CRDB Marathon walieleza kuwa tukio hilo la kila mwaka limekuwa na mchango mkubwa si tu katika kuhamasisha mazoezi na afya bora kwa jamii, bali pia katika kuchangia miradi ya kijamii kupitia fedha zinazokusanywa kutokana na mbio hizo.

Ushiriki wa TPDC Runners Club katika marathon hii ni sehemu ya utekelezaji wa sera za Shirika katika kujali afya za wafanyakazi, kuchangia maendeleo ya jamii na kudumisha mshikamano kupitia michezo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...