Na Mwandishi Wetu Michuzi Tv 

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesisitiza kutekeleza agizo lake la kutoza kodi kwa biashara za mtandaoni, hususan huduma za malazi (online accommodation), ifikapo Septemba Mosi,mwaka huu 2025

Akizungumza  jijini Dar es Salaam leo Agosti 9, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya elimu ya kodi kwa biashara za mtandaoni, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, amesema licha ya muda wa usajili kuhitimishwa Agosti 31, baadhi ya wadau wamelalamika muda huo kutotosha na kuomba uongezwe.

Hata hivyo, TRA itatekeleza agizo hilo kama lilivyoelekezwa, kufuatia mabadiliko ya kifungu cha 51 cha Sheria ya Kodi, kitakachoanza rasmi Septemba 1 mwaka huu, kwa wamiliki wa mali za majengo yanayotoa huduma za malazi wanaotumia majukwaa ya mtandao.

Masharti hayo hayatahusu wafanyabiashara wadogo wanaotumia mitandao kwa kujitangaza, kwani wameongezewa muda.

Mwenda amesema TRA imeongeza muda kwa wafanyabiashara wadogo wanaotumia mtandao kujitangaza, ili kuwapa nafasi ya kupata elimu ya kutosha, kushiriki semina na kusajiliwa, ambapo mchakato wote utafanyika kwa njia ya mtandao.

“Hatuna nia ya kuua biashara zenu. Kazi yetu ni kuwezesha biashara. Pale ambapo mnapata changamoto za kupata faida, ni wajibu wetu kuwasaidia ili muendelee kufanya biashara zenu,” amesema Mwenda.

Aidha, Mwenda amesema TRA imejipanga kutumia teknolojia kuwatambua wafanyabiashara wote wa mtandaoni na itahamasisha wanunuzi kutoa taarifa kwa mamlaka pale ambapo hawapati risiti, ambapo taarifa sahihi zitazawadiwa asilimia tatu ya kodi itakayokusanywa.

“Lengo ni kuwezesha na kurasimisha biashara zenu, ili muweze kukopesheka, kutonyanyaswa na kushindana kimataifa,” ameongeza.

Amesema hatua hiyo inalenga kupanua wigo wa ukusanyaji kodi ili kupunguza malalamiko ya viwango vya kodi na kuweka viwango thabiti, hivyo kuiwezesha serikali kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi.

Kuhusu malalamiko ya risiti za EFD, Mwenda amesema sasa kuna mfumo mpya wa VFD unaotumia programu za simu, ambao ni rahisi zaidi.

Akijibu malalamiko kutoka kwa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuhusu sheria ya kupiga marufuku biashara fulani kwa wageni, Mwenda amesema hatua hiyo inalenga kulinda biashara za Watanzania na viwanda vya ndani.

Pia, kuhusu wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa wanaotegemea bidhaa kama saruji kutoka nchi jirani, Mwenda amesema TRA inaendelea kufanya tathmini na mazungumzo ya pande mbili kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), John Daffa, amesema sekta ya mawasiliano ni nyenzo muhimu katika uchumi wa kidijitali, hivyo TCRA itaendelea kutoa leseni na huduma za kuwezesha miundombinu imara ya mawasiliano, sambamba na kushirikiana na TRA katika kufanikisha biashara za mtandaoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) amesema baraza hilo liko tayari kushirikiana na TRA katika kutoa elimu kwa Watanzania, hasa wasanii, watengeneza maudhui na wamiliki wa mitandao ya kijamii, ili kurasimisha kazi zao na kulipa kodi.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanya Biashara wa Kariakoo, Severin Mushi, amesema TRA inapaswa kuwekeza zaidi katika elimu ya mlipakodi kuanzia shule za msingi, na ametoa wito kwa TCRA kuhakikisha huduma ya mtandao inapatikana kwa uhakika, akisema tatizo la kuzimwa kwa mtandao linaathiri biashara.




Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, akizungumza na wadau mbalimbali wa kodi wakati wa uzinduzi wa kampeni ya elimu kwa mlipa kodi, mabadiliko ya sheria za kodi 2025 na biashara za mtandaoni katika semina iliyofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 9,2025.
Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), John Daffa, akitoa maelezo kuhusu mchango wa sekta ya mawasiliano katika kukuza uchumi wa kidijitali wakati wa ufunguzi wa kampeni ya Elimu kwa mlipa kodi,  mabadiliko ya sheria za kodi 2025 na biashara mtandaoni.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanya Biashara wa Kariakoo, Severin Mushi, akitoa wito kwa TRA na TCRA kuboresha elimu ya mlipakodi na huduma za mtandao ili kuwezesha  wafanyabiashara kuendel3a kulipa kodi kwa hiari.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...