📌 Yaagiza malipo yafanywe haraka kupitia vyama vya ushirika
📌 Yasitisha makato ya bima ya tumbaku kupitia mikopo ya pembejeo
📌 Yaonya wanaochezea mizani za kidigitali
Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imeagiza wanunuzi wote wa tumbaku na pamba katika msimu wa masoko wa 2025/2026 kuhakikisha wanalipa fedha za mazao kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika haraka iwezekanavyo, kufuatia malalamiko ya ucheleweshaji wa malipo katika mikoa mbalimbali.
Uchunguzi wa Tume umebaini kuwa baadhi ya makampuni ya ununuzi wa tumbaku yamekuwa yakichelewesha malipo bila sababu za msingi, hali inayosababisha usumbufu mkubwa na kuathiri ustawi wa wakulima wa zao hilo.
Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Tume, Dkt. Benson Ndiege, amesema vyama vya ushirika vinapaswa kuwalipa wakulima wote wanaodai mara tu fedha zinapopokelewa, huku taasisi za fedha zikielekezwa kuweka wazi riba za mikopo wanazotoa kwa vyama hivyo. Aidha, Serikali imesitisha makato ya gharama za bima ya zao la tumbaku kupitia mikopo ya pembejeo hadi utaratibu mpya utakapowekwa.
Kuhusu matumizi ya mizani za kidigitali, Ndiege amesema jumla ya mizani 4,634 yenye thamani ya shilingi bilioni 15.16 imesambazwa kupitia vyama vya ushirika hadi Juni 2025. Hata hivyo, kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa wakulima wa pamba kuhusu usahihi wa vipimo, ambapo uchunguzi umebaini hujuma zinazofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika.
Serikali imeagiza bodi zote za AMCOS ambazo hazijachukua hatua dhidi ya wahusika zifanye hivyo mara moja, na kushirikiana na mamlaka za mikoa kuhakikisha wanaohujumu mizani wanaondolewa madarakani na kufikishwa kwenye vyombo vya dola.
Ndiege ameonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kuchezea au kuharibu mizani za kidigitali zinazotumika kupima mazao ya wakulima atakabiliwa na hatua kali za kisheria.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...