Vodacom Tanzania PLC imesaini ushirikiano na Shirika la Salesian of Don Bosco Kanda ya Tanzania na kuzindua mfululizo wa mipango inayolenga kuwawezesha vijana na kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu jijini Dar es Salaam. Ushirikiano huu umehalalishwa kupitia kusainiwa kwa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU), yakionyesha udhamini rasmi wa Vodacom kwa Don Bosco na Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL).

Tukio la uzinduzi limeangazia dhamira ya Vodacom katika kuwawezesha vijana, kujiendeleza kielimu na michezo, kwa lengo la kukuza vipaji vya ndani na kuimarisha maendeleo ya jamii.

Kama sehemu ya mpango huu, Vodacom imekarabati uwanja wa mpira wa kikapu wa Don Bosco Oysterbay, na kutengeneza mazingira salama na ya kisasa kwa wanamichezo chipukizi kujifunza na kushindana. Zaidi ya hayo, Vodacom imefadhili masomo ya wanafunzi 80 katika vipindi tofauti vya elimu katika Chuo cha Ufundi cha Don Bosco Oysterbay, ili kuwasaidia katika maendeleo yao ya kitaaluma na binafsi.

Akizungumza katika tukio hilo, Bi. Zuweina Farah, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania PLC alisema, "uwekezaji wetu ni zaidi ya kwenye michezo, tumejikita katika kukuza uwezo wa vijana kupitia elimu na ushirikiano wa kijamii. Kwa kufadhili masomo na kuboresha miundombinu ya michezo, tunalenga kutengeneza fursa zitakazowahamasisha na kuwawezesha vijana."

Vodacom pia inalenga kuimarisha uhusiano wake na kundi la vijana kupitia majukwaa kama VYB, kwa kuongeza ushiriki wa chapa na uelewa, "udhamini huu ni sehemu ya mkakati wetu wa kuungana na soko la vijana, tukionyesha kujitolea kwetu katika ukuaji na mafanikio yao," aliongeza Bi. Farah.

Padri Emilius Salema, Mkuu wa Shirika la Salesian of Don Bosco, Kanda ya Tanzania, aliishukuru Vodacom Tanzania kwa msaada wake, “tunatoa shukrani za dhati kwa Vodacom Tanzania kwa mchango wao mkubwa. Ukarabati wa uwanja wetu wa mpira wa kikapu na ufadhili wa masomo uliotolewa utakuwa na matokeo chanya ya muda mrefu kwa wanafunzi wetu na jamii kwa ujumla. Ushirikiano huu utawahamasisha wanamichezo wetu chipukizi na wanafunzi kujifunza na hivyo kuwa bora zaidi."

Bi. Farah alisisitiza tena dhamira ya Vodacom kwa jamii ya mpira wa kikapu, “tunajivunia kuunga mkono BDL na kuchangia katika ukuaji wa mpira wa kikapu nchini Tanzania. Ushirikiano huu unaakisi dhamira yetu pana ya kuleta athari chanya katika jamii na kujenga mahusiano ya kudumu na vijana wa Kitanzania."

Rais wa chama cha Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL), Bw. Shendu Hamis Mwagalla, naye alitoa shukrani zake, "tunaishukuru Vodacom Tanzania kwa udhamini na msaada wao. Ushirikiano huu utaikuza ligi, kuendeleza wachezaji wetu na kuhamasisha mpira wa kikapu kote Dar es Salaam. Tunatarajia msimu wenye mafanikio na ushirikiano endelevu."

Vodacom Tanzania inaendelea kujitolea kuleta mabadiliko chanya katika jamii inazozihudumia, kwa kutumia michezo na elimu kama nyenzo madhubuti za maendeleo.

Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah (kulia), na Mkurugenzi wa TEHAMA wa kampuni hiyo, Athumani Mlinga (kushoto), wakimkabidhi tuzo mchezaji wa Don Bosco, Martin Benson, aliyechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi. Tukio hilo, lililofanyika tarehe 29 Agosti katika viwanja vya Don Bosco jijini Dar es Salaam, liliambatana na utiaji saini wa makubaliano kati ya Vodacom Tanzania na Shirika la Salesians of Don Bosco kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa mpira wa kikapu na kusaidia ufadhili wa masomo.
 Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah (aliyesimama kulia), akikabidhi mpira kwa Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu mkoa wa Dar es Salaam, Shendu Mwagala, kama ishara ya makubaliano ya kuendeleza mchezo huo jijini hapo. Tukio hilo, lililofanyika tarehe 29 Agosti katika viwanja vya Don Bosco, lilishuhudiwa na Mkuu wa Shirika la Salesians of Don Bosco Kanda ya Tanzania, Padre Emilius Salema (kushoto), pamoja na Mchezaji Bora wa Muda Wote (MVP), Baraka Sadick.
Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah (wa pili kulia), akiwa kwenye picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, Shendu Mwagala (kushoto), Padre Emilius Salema wa Salesians of Don Bosco (wa pili kushoto) na Mchezaji Bora wa Muda Wote (MVP), Baraka Sadick. Tukio hilo la utiaji saini wa makubaliano ya kuendeleza mpira wa kikapu na kufadhili elimu limefanyika tarehe 29 Agosti kwenye viwanja vya Don Bosco jijini Dar es Salaam.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...