Na Beatus Maganja,Dar es Salaam

Walimbwende 24 wanaoshiriki mashindano ya Miss Grand Tanzania 2025 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara, wamefanya ziara ya siku moja katika Hifadhi ya Pande iliyopo jijini Dar es Salaam tarehe 13 Agosti 2025 kwa lengo la kujifunza masuala ya uhifadhi na utalii wa ndani.

Ziara hiyo iliandaliwa kwa ushirikiano kati ya waandaaji wa Miss Grand Tanzania na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha walimbwende hao kujifunza masuala ya uhifadhi na utalii na kuwa mabalozi wa vivutio vya utalii wa ndani, hususan Hifadhi ya Pande.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kaimu Kamanda wa Hifadhi ya Pande, PC Suleiman Keraryo, alisema hifadhi hiyo ni kivutio cha kipekee kilichopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo wageni hupata fursa ya kutalii na kujionea vivutio mbalimbali  ikiwa ni pamoja na kujifunza kuhusu historia ya hifadhi hiyo, bioanuwai na mchango wake katika uhifadhi wa mazingira na viumbe hai.

“Karibuni sana katika Hifadhi yetu ya Pande, hifadhi iliyo katikati ya Jiji la Dar es Salaam, ikiwa na wanyamapori wa aina mbalimbali na vivutio vingine lukuki. Hapa ni mahali sahihi kwenu kujifunza na kujionea rasilimali za nchi yenu,” alisema Keraryo.

Aidha, alibainisha kuwa mshindi wa Miss Grand Tanzania 2025 atateuliwa kuwa Balozi wa Hifadhi ya Pande, ambapo atashirikiana na TAWA katika juhudi za kuitangaza hifadhi hiyo pamoja na kuchochea utalii wa ndani, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya maliasili na utalii.

Mashindano ya fainali ya Miss Grand Tanzania yanatarajiwa kufanyika tarehe 16 Agosti 2025 katika Ukumbi wa Superdome, Masaki – Dar es Salaam.

Uongozi wa Hifadhi ya Pande pia umeeleza dhamira yake ya kuendeleza ushirikiano na waandaaji wa Miss Grand Tanzania kwa kuhakikisha kuwa walimbwende wanapata fursa ya kulala ndani ya hifadhi hiyo na kufanya mazoezi katika mazingira ya asili, ili kuongeza uelewa wao kuhusu uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wao, walimbwende wameeleza kufurahishwa na ziara hiyo, hususan kupata fursa ya kuona kwa ukaribu aina mbalimbali za wanyamapori waliopo hifadhini humo, sambamba na mapokezi mazuri kutoka kwa maofisa wa TAWA. Pia waliahidi kuwa mabalozi wa kuitangaza hifadhi hiyo kwa jamii.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa ni mwanzo wa ushirikiano endelevu kati ya TAWA na taasisi za kijamii, hususan zinazowalenga vijana, kwa lengo la kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kulinda mazingira na kuendeleza utalii wa ndani kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...