Na Diana Byera - Muleba.

Serikali Mkoani Kagera kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeahidi kuendelea kuongeza vitendea kazi na kubuni teknolojia wezeshi kwa ajili ya kuwafikia wananchi wote waliokosa fursa ya kupata elimu kwa mfumo rasmi, Lengo ni kuwawezesha kupata maarifa na ujuzi utakaosaidia kupambana na maadui watatu wa maendeleo yaani umasikini, ujinga na maradhi.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Muleba katika kilele cha maadhimisho ya juma la elimu ya watu wazima, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bwai Mashauri, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, alisema kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, asilimia 3.3 ya wakazi wa mkoa huo hawajui kusoma wala kuandika.

Mashauri amesema kuwa mkoa kupitia Idara ya Elimu ya Watu Wazima unaendelea kuweka miundombinu wezeshi na kutoa ushawishi kwa kila mtu aliyeikosa elimu ya awali kupata fursa ya kujifunza bila kujali umri, hata akiwa amefikisha miaka 60, ili kupunguza umasikini na kuhakikisha usawa wa fursa katika jamii nzima.

Amefafanua kuwa mfumo wa elimu ya watu wazima unahusisha kuwafundisha kusoma na kuandika, kuwajengea uwezo wa ubunifu wa bidhaa, ujasiriamali, uzalishaji mali, pamoja na kuwaunganisha katika masoko ili kuondoa tofauti zilizopo baina ya waliopata elimu rasmi na wale ambao hawakuwahi kupata.

Amesema Kwa mwaka 2025, watoto 402 waliokuwa wamekosa elimu ya msingi waliweza kujiunga kwenye mfumo rasmi wa elimu baada ya kufundishwa kusoma, kuandika na kuhesabu.

Aidha mkoa uliwezesha vikundi 3,450 kupata ujuzi wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kwa ubunifu, hatua iliyosaidia kuongeza kipato cha familia nyingi zilizojifunza stadi za maisha kupitia elimu ya watu wazima.

Kupitia maadhimisho hayo, Mashauri ametoa wito kwa maafisa elimu kata kushirikiana na watendaji wa vijiji na mitaa kuweka sheria ndogo ndogo zitakazowezesha kila mwananchi kupata elimu bila kujali umri wake. Alisisitiza kuwa elimu ni chombo kikuu cha kutokomeza umasikini unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa elimu.

"Natoa wito kwa wanaoendesha mifumo ya elimu ya watu wazima kuhakikisha kuna vipengele vinavyovutia. Watu wazima wengi hukwepa kujifunza kusoma na kuandika, lakini wanapovutiwa na ujuzi wa kutengeneza bidhaa zitakazowaingizia kipato, hujitokeza kwa wingi na kujifunza. Kupitia njia hiyo, mtu mmoja hupata elimu ya kusoma na kuandika, ujasiriamali na ujuzi wa maisha hivyo kupambana na maadui watatu kwa wakati mmoja," alisema Mashauri.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Kagera, Honoratha Kabundunguru, alisema kuwa hadi sasa mkoa una vituo 132 vinavyotoa elimu ya watu wazima kwa rika zote.

Alieleza kuwa watoto wa mtaani wapatao 4,061 waliandikishwa kupatiwa elimu ya msingi ya kusoma, kuandika na kuhesabu, ambapo kati yao, watoto 3,891 sawa na asilimia 96 walifaulu na sasa wanajiunga na mfumo rasmi wa elimu, asilimia 4 waliobaki wanaendelea na masomo hadi watakapofaulu.

Changamoto kubwa zilizobainishwa ni ukosefu wa vitendea kazi katika vituo vya elimu ya watu wazima, walimu wengi kujitolea bila malipo, jamii kutoonyesha ushirikiano katika kutoa taarifa kuhusu watoto walioko mitaani, kutotimiza wajibu kwa baadhi ya walezi, ajira za utumikishwaji wa watoto majumbani, pamoja na wanafunzi wa kike wanaorejea shuleni baada ya mimba kukumbana na changamoto za kitaaluma.

Idara ya Elimu imeomba mpango wa kutoa elimu ya sekondari kwa njia mbadala kwa wasichana waliokatiza masomo kutokana na ujauzito au matatizo mengine kuangaliwa upya, kwani ufadhili wake unatarajiwa kuisha mwaka 2026. Hii ni ili kuwawezesha wasichana hao kupata nafasi ya kuendelea na elimu au kupata ujuzi kupitia mifumo mingine.

Maadhimisho hayo yalitoa fursa kwa wahitimu wa elimu ya watu wazima kuonyesha bidhaa walizotengeneza kwa mikono yao kwa muda wa siku nne mfululizo, kutoa ushuhuda juu ya umuhimu wa elimu, kupatiwa vyeti, pamoja na kuunganishwa na mifumo ya kifedha na masoko ili kukuza uchumi wao binafsi na wa familia zao.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...