Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mchinga

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewaambia wananchi wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi kuwa  iwapo Chama hicho kitapewa ridhaa kuendesha serikali itakwenda kukamilisha miradi iliyoanzishwa na ile iliyoahidiwa kupitia Ilani ya uchaguzi.

Dk.Samia ameyasema hayo  leo Septemba 25,2025 alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi akiwa katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.

"Tumerejea tena kuomba ridhaa tuendelee twende tukatekeleze ilani tuliyoileta kwenu ya mwaka 2025 - 2030 na sina wasiwasi kwa ujumla kama mkoa na jimbo hili. Najua mkoa wa lindi mmezima zote mmewasha kijani," amesema.

Amesema endapo CCM ikipewa ridhaa kuendesha serikali itakwenda kukamilisha miradi iliyoanzishwa na ile iliyoahidiwa kupitia Ilani ya uchaguzi.

Amesema kwa upande wa maji serikali imeshakamilisha awamu ya kwanza ya mradi ambapo awamu ya pili utakwenda kunufaisha vijiji vingine 10 vya jimbo hilo ambavyo havijapata maji.

Ameongeza kuwa lengo la serikali ni kuona wananchi wa jimbo hilo wananufaika na huduma za maji safi na salama huku akisisitiza akipewa ridhaa ya kuongoza serikali, visima vitachimbwa katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo kwa lengo la kuongeza kasi ya upatikanaji maji.

Kuhusu kilimo, Dk.Samia amewahakikishia wananchi serikali yake itaendelea kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo."Tutaleta suphur bure, dawa za kuua wadudu lakini dawa za kukabiliana na magonjwa ya mazao bure ili mikorosho ilimwe na uzaliwe kwa wingi.

"Tunafanya hivyo ili kujenga uwezo wa mkulima, tungemtaka mkulima afanye kila kitu mwenyewe, mazao ambayo mkulima ameyapata yasingeweza kupatikana.Mashamba yasingekuwa yanapewa huduma inayostahili. 

“Tunatoa ruzuku ili mkulima apate kuhudumia mashamba vizuri, korosho izaliwe, fedha iingie nyingi ili aweze kusimama mwenyewe,”amesema Dk.Samia na kuongeza Serikali  inaendelea kutafuta masoko yenye uhakika ambapo mfumo wa stakabadhi ghalani umetoa matokeo mazuri.”

Pia amesema  mfumo huo ulikuwa mgumu kukubalika lakini umeleta matokeo mazuri kwa wakulima."Nataka niwahakikishie kwamba, kinacholetwa na serikali yenu mjue kina manufaa. Kikubalieni na mkifanyie kazi.

Ameongeza kuwa Serikali inatoa  huduma za kitaalamu, huduma za ugani kuwawezesha maofisa ugani waweze kufuatilia maendeleo ya kilimo chetu.Serikali imetoa fedha kutekeleza miradi miwili ya umwagiliaji katika maeneo ya Lutamba na Kilangala.

Dk. Samia amesema  hatua hiyo itawawezesha wakulima katika maeneo hayo kuzalisha mazao yao mara mbili kwa mwaka.Kwasasa  nchini hakuna mazao ya biashara na chakula kwani hata mazao ya chakula nayo yamekuwa mazao ya biashara.

"Tunalisha majirani zetu, huko nyuma mbaazi hapa Lindi ilikuwa mboga lakini leo mbaazi ni zao la biashara na linaingia katika stakabadhi ghalani likitea bei nzuri kwa hiyo tutaendelea kufanya kilimo cha umwagiliaji ili watu wazalishe mara mbili kwa mwaka.

Amesema kuwa kwasababu hata mpunga ni zao la kibiashara huku akifafanua Mpunga wetu upo nchi nyingi za Afrika Mashariki hata Ulaya mchele wa Tanzania unapatikana.

Pamoja na hayo Serikali itaendelea kusimamia sekta ya kilimo kwa sababu Tanzania inazalisha mazao kwa wingi hivyo muhimu kuwepo upatikanaji masoko yenye uhakika.

Ametoa ahadi kwa wananchi wa jimbo hilo kwamba serikali itajenga soko litakalo hudumia mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga.

“Lengo ni kwamba ujenzi wa skimu za umwagiliaji utakapokamilika, wakulima watafundishwa walime mazao ya mbogamboga ambayo nayo yanauzwa nje ya nchi.”



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...