Kassim Nyaki, Karatu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi amefungua mafunzo ya siku tatu kuhusu elimu ya utalii wa anga (astrotourism) yaliyoanza leo tarehe 19 Septemba, 2025 Karatu Mkoani Arusha.
Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) yanatolewa na wataalamu wabobezi kutoka taasisi za Astrotourism Aotearoa (AAA) kutoka nchini New Zealand, Smithsonian Astrophysical Observatory (SAO) ya Chuo Kikuu cha Harvard pamoja na taasisi ya kimataifa ya Dark Sky International yenye Makao Makuu Jijini Arizona, Marekani.
Akifungua mafunzo hayo Dkt. Abbas amesema utoaji wa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Wizara ya Maliasili na utalii kufungua mazao mapya utalii ikiwepo utalii wa Anga ambapo hatua ya sasa ni kutoa mafunzo, maarifa na ujuzi kwa watanzania kuhusu utalii wa anga, vifaa vinavyotumika na fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu huria cha Tanzania Prof. Saganga Kapaya ameeleza kuwa Tanzania inazo fursa nyingi za utalii wa anga, ambao ni bidhaa mpya ya utalii hapa nchini kwa kuwa zaidi ya theluthi moja ya ardhi ya Tanzania imehifadhiwa, na hivyo kupelekea maeneo yake mengi kuwa na anga lenye giza wakati wa usiku hivyo kuwezesha anga kuonekana kwa zaidi ya asilimia 95 ukilinganisha na mataifa mengine Afrika.
Prof. John Hearnshaw kutoka New Zeland ambaye ni mwezeshaji wa mafunzo hayo ameeleza kuwa mafunzo yatajikita katika maeneo manne ambayo ni namna ya kuendesha utalii wa anga kwa kushirikisha wadau wa utalii na Jamii, utalii wa anga na Fizikia anga, matumizi ya Telescopic pamoja na upigaji wa picha za utalii wa anga.
Mafunzo hayo yamehudhuriwa na washiriki zaidi ya 70, ambao ni wasafirishaji watalii (Tour Operators), waongoza watalii (tour guides), waendeshaji wa huduma za malazi (Hoteliers ), taasisi za serikali zinazohusika na kutangaza utalii (TTB na ZCT), taasisi za uhifadhi (NCAA, TANAPA, TAWA, na TFS), taasisi za elimu, mafunzo na utafiti (NCT, ACWM-Mweka, VETA, na OUT), Wataalamu wa Utalii, Wasimamizi wa Utalii, Watafiti, Waandaaji wa sera na wafanya maamuzi, Wana-astronomia, Wanafunzi, Wajasiriamali, na watunga sera.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...