Na Said Mwishehe,Singida.

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Rais Dk.Samia Suluhu amesema moja ya ahadi ya Serikali kwa wananchi wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida ilikuwa ni uanzishwaji soko la madini ambalo limeshaanzishwa eneo la Shelui hivyo ametoa rai kwa  vijana kuchangamkia fursa.

Dk.Samia ameyasema hayo leo Septemba 10,2025 alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi wa Iramba Mkoa wa Singida ambapo amesema kumekuwa na mafanikio makubwa ya utekelezaji wa Ilani iliyopita 

“Serikali iliahidi uanzishwaji wa soko la madini na leo tumekuja kuomba kura kwa ujasiri kwasababu Ilani iliyopita imetekelezwa vizuri.Katika soko la Madini ambalo limeanzishwa zaidi ya gramu milioni 1.5 zimeuzwa kwa thamani ya sh. bilioni 192.

"Sh. bilioni 192 zimeingia mikononi mwa wachimbaji ndani ya wilaya hii. Soko lile linaendelea kutoa huduma.Niwaombe wachimbaji tumeweka soko lile ili dhahabu inayochimbwa, vito vinavyopatikana viuzwe ndani ya soko badala ya kuchepusha na kuipeleka nje bila kuuza ndani ya nchi," amesema.

Pia amesema serikali iliahidi kutoa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo ambapo tayari maeneo yaliyohodhiwa na waliokuwa hawayatumii leseni zake zimefutwa.

Amefafanua  leseni hizo zilifutwa kisha kugawiwa upya kwa wachimbaji ambapo leseni 32 zimetolewa kwa vikundi tisa ndani ya Wilaya ya Iramba kwa wachimbaji wadogo wa madini.

“Leseni nane za uchenjuaji madini ya dhahabu zimetolewa katika eneo la Sekenke.Hiyo yote ni kuhakikisha vijana wetu ndani ya Singida wanapata ajira za kutosha iwe kwenye kilimo, miradi, iwe kwenye madini au kokote kule vijana wapate ajira za kutosha," alisisitiza.

Dk. Samia alisema kuhusu mradi wa bomba la gesi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, mradi huo unapita ndani ya Mkoa wa Singida.

Alisema mradi huo unaleta ajira kwa vijana, hivyo alitoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa."Mkiziacha watakuja vijana wa mikoa jirani wachukue fursa hizo na nyinyi mbaki mnatizama," amesema Dk.Samia.

Kwa upande wa Iramba Mashariki alisema serikali itakamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa umwagiliaji katika Kijiji cha Ishishi, Kata ya Msingi kwa gharama ya sh. bilioni 34.

Alisema lengo ni wakulima walime mara mbili kwa mwaka.

"Tulipokuwa tunategemea mvua ya Mwenyezi Mungu wakulima walikuwa wanalima mara moja kwa mwaka lakini sasa watakwenda kulima mara mbili kwa mwaka," Dk. Samia alieleza.

Pia  anafahamu kuna uhitaji kuufungua mji wa Kiomboi kwa kuimarisha mawasiliano kati ya Wilaya ya Iramba na Mkalama.

Hivyo, amesema  serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara za Iguguno mpaka Sibiti na barabara ya Kiomboi hadi Mtulia.

Pamoja na hayo amesema CCM ina mipango mikubwa ya kuchochea maendeleo ya nchi yetu, hivyo ametoa rai kwa wananchi kujitokeza Oktoba 29 kukichagua Chama Cha Mapinduzi kwani kwa wingi wa wananchi wanaofika uwanjani ndio huo huo unatarajiwa kwenye masanduku ya kura.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...