.jpg)
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Muheza (CCM) Hamisi Mwinjuma alimaarufu Mwana FA amesema hana wasiwasi na watu wa Tarafa ya Amani na wilaya ya Muheza isipokuwa amewaomba kila atakayekwenda kupiga kuwa Octoba 29 amchukue na mwenzake ili wilaya hiyo iongoze kwa kura nyingi za Rais na Madiwani wa CCM katika Kata 37 za Muheza waweze kushinda akiwemo yeye.
Mwana FA aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kampeni zake za Ubunge zilizofanyika Septemba 10 katika Kijiji cha Bulwa tarafa ya Amani ambapo MwanaFA alisema wananchi wa Muheza waendelee kukiamini chama hicho na wagombea wake kwa kuwa katika miaka mitano iliyopita wameweza kutekeleza ilani ya uchaguzi kwa kiwango kikubwa.
.jpg)
Alisema kimsingi wapinzani waliopo kwa Sasa wanaogombea nafasi mbalimbali za uongozi, wameishiwa na hawana hoja na tena wangetamani kuwa wagombea wa CCM lakini hawakuweza kutokana na ushindani uliokuwepo kwenye chama hicho.
“Naombeni mnipigie kura na wagombea udiwani wa CCM kwakuwa mimi siyo mbunge mpya bali ni sheikh yule yule isipokuwa kanzu mpya na nimedhamiria kutatua changamoto za wilaya hii nikiwa mwakilishi wenu kwakuwa miaka mitano iliyopita tumeshirikiana vema na wananchi na tumetekeleza miradi mingi yenye tija”Alisema Mwana FA.

Mgombea huyo alisisitiza umuhimu wa wananchi kuhakikisha wanampa kura nyingi za kutosha wagombea wa CCM akiwemo Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuhakikisha wilaya ya Muheza inaongoza ili waendelee kushirikiana kuleta maendeleo.

Amesema kwamba serikali imeanza kufanyia kazi na amewahakikishia wawekezaji wote wilayani Muheza,ambao wamehodhi mashamba pamoja na viwanda ambavyo hawajavifanyia kazi, watanyang'anywa na kurejeshwa kwa wananchi ili wayafanyie shughuli zao za kiuchumi.
Alisema kila jambo ambalo ni changamoto wilayani humo ameaahidi anakwenda kuyafanyia kazi kama ambavyo miaka mitano iliyokwisha amefanya na kutekelezaji miradi mingi ya maendeleo.
Awali diwani wa kata ya Misalai Said Mtunguja akizungumza kwa naiba ya madiwani wote walioshiriki uzinduzi huo, alisema kuwa hawana deni la mbunge Wala Rais Dkt Samia kwa namna walivyoshirikiana kutatua changamoto kwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo elimu, afya, miundombinu pamoja na huduma za jamii.
Diwani huyo alisema kwamba kwa sasa tarafa hiyo changamoto pekee iliyokuwepo ni suala la wafanyakazi wa kampuni ya chai ya Usambara Mashariki (EUTCO) kukabiliwa na tatizo la kukosa mishahara kwa wakati.
Alisema wafanyakazi hao wanaweza kukaa miezi mitatu hadi minne hawalipwi mishahara yao na kufanya maisha kwa upande wao kuwa magumu ikiwemo kukabiliwa na madeni mitaani.
Pia alisema kuwa kutokana na kata hiyo kuzungukwa na mashamba makubwa ya chai, serikali ingewasaidia wananchi kupata maeneo ambayo mwekezaji ameshindwa kuyaendeleza wapewe wananchi wafanye Makazi pamoja na mashamba ya kulima.
Mapema mgeni rasmi katika mkutano huo, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Tanga, Nassor Makau aliyemwakilisha Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah aliwataka wananchi wa Muheza kuwachagua wagombea wa CCM kwa kuwa Chama hicho kimekuja na ilani inayotekelezeka.
Alisema wananchi Wana Kila sababu ya kuwachagua wagombea wa CCM kwakuwa katika kipindi cha miaka mitano miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kimkakati imetekelezwa kwa kiwango kikubwa katika mkoa wa Tanga na Muheza kwa ujumla.
Amewaomba wananchi wampigie kura mgombea Urais wa Chama hicho Dkt Samia Suluhu Hassan, mbunge pamoja na madiwani ili waweze kushirikiana kuleta maendeleo na kamwe wasiwachague wagombea wa upinzani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...