NA MWANDISHI WETU

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Umahiri cha Usalama Barabarani (Regional Center of Excellence for Road Safety) katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ni hatua kubwa ya kitaifa na kikanda katika mapambano dhidi ya ajali barabarani.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo leo18,2025 chuoni hapo, Mhandisi Besta amesema kituo hicho kimeanzishwa kwa lengo la kutoa weledi na kuweka mipango ya kitaalamu ya kuimarisha usalama barabarani nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Kituo hiki si cha kitaifa pekee, bali ni cha kikanda. Kitajikita katika kujenga uwezo wa wataalamu, kufanya tafiti na kusaidia katika kutoa maamuzi kwa kutumia takwimu. Lengo letu ni kuhakikisha tunapunguza maafa ya ajali, kwa kuzingatia pia utekelezaji wa maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu usalama barabarani,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema kituo hicho kimeanzishwa kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza ajali.

“Regional Center of Excellence ni jukwaa la kikanda litakaloshughulika na tafiti, mafunzo, kampeni za uhamasishaji na kutoa ushauri elekezi. Tutahakikisha usalama barabarani unazingatiwa kuanzia usanifu wa barabara, ujenzi hadi matumizi yake. NIT itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha ajali zinapungua kwa kiwango kikubwa,” amesema Dkt. Mgaya.

Naye, Mhandisi Kashinde Mussa, Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Wizara ya Ujenzi na Mwenyekiti wa Bodi iliyozinduliwa, amesema jukumu kubwa la Bodi hiyo ni kusimamia matumizi ya teknolojia katika kupunguza ajali.

“Takwimu zinaonyesha kuwa ajali nyingi nchini zinasababishwa na mienendo ya kibinadamu. Utafiti wa mwaka 2007 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam unaonesha kuwa asilimia 76.1 ya ajali chanzo chake ni tabia za binadamu. Kupitia Bodi hii, tutawekeza zaidi kwenye teknolojia na ushauri wa kitaalamu ili kupunguza ajali kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Bodi hiyo shirikishi inatarajiwa kusimamia utekelezaji wa shughuli za Kituo cha Umahiri cha Usalama Barabarani na kuhakikisha maazimio ya kitaifa na kimataifa kuhusu usalama barabarani yanatekelezwa ipasavyo.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...