*Mhe. Mary Maganga aimwagia sifa, Mkurugenzi Mkuu NSSF atoa siri ya mafanikio
Na MWANDISHI WETU,
Kigoma. Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umepongezwa kwa mafanikio makubwa ya utendaji yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2024/25 kwa kufikisha thamani ya shilingi trilioni 9.9 kutoka trilioni 8.3 mwaka wa fedha 2023/24.
Pongezi hizo zimetolewa tarehe 24 Septemba, 2025 na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Mary Maganga wakati akifungua mkutano wa 55 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa NSSF uliofanyika Mkoani Kigoma.
Alisema mafanikio hayo yametokana na usimamizi bora, matumizi ya TEHAMA na udhibiti wa mianya ya upotevu wa mapato. “Ni wajibu wenu kuendelea kuboresha huduma kwa wanachama kupitia TEHAMA, kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na kuongeza ubunifu katika kuwafikia wanachama wapya,” alisema Mhe. Mary huku akiwataka waajiri kuwasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati kwa kuwa ni takwa la kisheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Bw. Masha Mshomba alisema mafanikio hayo yametokana na Mfuko kufanikiwa kufikia malengo yake waliyojiwekea katika mwaka wa fedha 2024/25, hususan matumizi ya TEHAMA, kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa michango.
Alisema mafanikio haya yametokana na dira ya Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, usimamizi thabiti wa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na mshikamano wa wanachama, waajiri na wadau.
“Katika mwaka wa fedha 2025/26 tumejiwekea lengo la kuongeza thamani ya Mfuko hadi kufikia shilingi trilioni 11.7,” alisema Bw. Mshomba.
Aidha, Bw. Mshomba alitaja changamoto zinazoukabili Mfuko kuwa ni baadhi ya waajiri kushindwa kuwasilisha michango ya wafanyakazi kwa wakati, hali inayosababisha usumbufu kwa wanachama wanapostaafu. Hata hivyo, alisema NSSF kwa kushirikiana na Serikali na taasisi nyingine za umma inaendelea kuhakikisha changamoto hizo zinapunguzwa.
Katika kuimarisha huduma, alisema kipaumbele kitaendelea kutolewa kwenye mifumo ya TEHAMA, ukusanyaji wa michango, ongezeko la mapato na mbinu za kuvaa viatu vya wateja ili kuhakikisha kila mwanachama anapata huduma bora na stahiki zake kwa wakati.
Akitoa neno la shukrani, Meneja wa NSSF Mkoa wa Kinondoni, Bw. Large Materu alimhakikishia mgeni rasmi kuwa maagizo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa bidii na weledi.
“Tutaendelea kuboresha mifumo ya TEHAMA, kuongeza ubunifu na kusimamia stahiki za wanachama ili kuhakikisha Mfuko unazidi kupiga hatua kubwa zaidi,” alisema Materu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...