-Globalmedicare yapongezwa kwa uratibu mzuri

Na Mwandishi Wetu

MADAKTARI bingwa wa hospitali tano nchini wanatarajiwa kufanya kambi ya wiki moja nchini Comoro ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilotoa wakati wa ziara yake visiwani humo.

Hospitali tano zitakazoshiriki kambi ya mwaka huu ni Benjamin Mkapa ya mkoani Dodoma, Hospitali ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Saratani ya Ocean Road, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa na Ubongo (MOI).

Madaktari watakaotoa matibabu hayo ni madaktari wa Moyo, Madaktari wa wanawake, madaktari wa saratani, madaktari wa mifupa na mishipa ya fahamu na madaktari wa figo.

Madaktari wengine ni wa mfumo wa mkojo, madaktari wa ngozi, mfumo wa maskio,pua na koo(ENT), meno na daktari wa mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Utalii Tiba, Dk Peter Kisenge ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakata Kikwete (JKCI).

Alisema Tanzania inategemewa zaidi na wananchi wa Comoro katika kupata huduma za sekta ya afya na kwamba idadi kubwa sana ya wananchi wa nchi hiyo wanakuja Tanzania kwa huduma mbalimbali.

Alisema baada ya Rais Samia kuona nchi hiyo ina uhitaji mkubwa wa madaktari bingwa wa magonjwa mbalimbali aliagiza madaktari bingwa wa Tanzania waende nchini humo kufanya kambi ya matibabu.

“Hii kambi ya Oktoba mwaka huu itafanyika katika mji wa Anjuan na mamlaka zote zinazohusika zinafanya maandalizi ya kwenda Comoro mwezi wa kumi ,” alisema

Naye Mratibu wa Kambi hiyo, Mkurugenzi wa Global Medicare, Abdulmalik Mollel alisema uamuzi wa Rais Samia kuagiza kufanyika kwa kambi hiyo ulitokana na mafanikio makubwa ya kambi ya madaktari bingwa wa Tanzania iliyofanyika nchini humo mwaka 2024.

Alisema kwenye kambi hiyo iliyofanyika mji wa Moron mwaka 2024 wananchi 2,700 walihudumiwa na madaktari bingwa bobezi kutoka hospitali tano za Tanzania

“Kwa ujumla mafanikio makubwa ya kambi iliyopita yalimfurahisha Rais na baada ya kuombwa na wananchi wa Comoro madaktari waende tena nchini humo aliridhia kambi kama ile ifanyike tena mwaka huu,” alisema Mollel

Alisema tayari Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Afya wamelifanyia kazi suala la kambi hiyo na wakala wa utalii tiba Global Medicare ndiyo inaratibu kambi hiyo kama ilivyofanya mwaka jana.

“Kambi itakuwa kuanzia tarehe 5 hadi 12 mwezi wa kumi itakuwa ya wiki moja itafanyika katika hospitali tatu za nchini humo na hospitali zetu tano zitashiriki kufanikisha kambi hiyo,” alisema

Molle alisema Wizara ya Afya kupitia Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe imeshatekeleza baadhi ya mambo na hospitali zitakazokwenda kule zimeshaarifiwa na zimeshateua madaktari watakaokwenda kule.

Mollel alisema tayari Wizara ya Afya imeshatuma timu ya watalaamu kutoka Tanzania kwenda nchini Comoro kwaajili ya maandalizi ya kambi hiyo ya wiki moja.

“Timu ya wataalamu kutoka Tanzania imeshaenda kule na kukutana na wawakilishi wa Serikali ya Comoro kupitia Balozi wa Tanzania nchini humo na wamekutana na wawakilishi wa hospitali tatu zitakazotumiwa na madaktaari wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa,” alisema .

Aidha, Mollel alisema wamezishirikisha taasisi kubwa za kimkakati kama Bohari Kuu ya Dawa (MSD) na kwenye kambi ya mwaka huu MSD itatoa washiriki kwenda kwenye kambi hiyo .

“Kwenye kambi ya mwaka huu kutakuwa na maonesho na vikao vya kujengeana uwezo baina ya madaktari wetu na wale wa Comoro na kutakuwa na mkutano baina ya Bohari Kuu ya Tanzania MSD na Bohari Kuu ya Dawa Comoro kubadilishana uzoefu,” alisema.

Alisema kwenye maandalizi ya kambi hiyo ya mwaka huu wameshirikisha viwanda vya dawa hapa nchini ili viangalie fursa ya kusambaza dawa za aina mbalimbali nchini humo.

Alisema matangazo yameshafanyika kwa wananchi wa Comoro ili wafahamu aina ya huduma ambazo madaktari wa Tanzania wanakwenda kuzitoa nchini humo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...