Na Mwandishi Wetu, Mwanza
TIMU za Ofisi za Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Shinyanga na Mwanza zimeng’ara kwa kufanya vyema kwenye michezo ya jadi katika michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) inayoendelea kwenye uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Wachezaji Omary Kadiba wa RAS Dar es Salaam na Badaka Kabaka wa RAS Mwanza wameshika nafasi ya pili kwenye mchezo wa fainali wa drafti kwa wanaume na wanawake; ambapo Kadiba alifungwa na bingwa Mohamed Ngorwe wa Wizara ya Maji kwa seti 1-0; huku Kabaka alifungwa na bingwa Salome Komba wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa seti 1-0.
Katika ushindi wa tatu kwa wanawake umechukuliwa na Janeth Mtawa wa Wizara ya Viwanda na Biashara aliyemshinda Janeth Sichone wa Wizara ya Ardhi kwa seti 2-1; wakati kwa wanaume ushindi wa tatu umekwenda kwa mkongwe Gervas Mwashimaha wa Wizara ya Maliasili na Utalii aliyemshinda Masoud Mwakoba wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa seti 2-0.
Katika mchezo wa karata kwa wanaume ubingwa umechukuliwa na Deus Paschal wa RAS Shinyanga, akifuatiwa na Edward Saimon wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wa tatu ni Ramadhani Kibwana wa Ofisi ya Ukaguzi; wakati bingwa kwa wanawake ni Amina Kaguru wa Wizara ya Maji, aliyefuatiwa na Severine Mnyaga wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na watatu ni Theresia Nungu wa RAS Shinyanga.
Katika mchezo wa kuvuta kamba kwa wanaume ushindi wa tatu umechukuliwa na Wizara ya Uchukuzi waliowavuta Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mivuto 2-0; huku kwa wanawake Mahakama waliwavuta kwa mbinde RAS Geita kwa mvuto 1-0.
Kwa upande wa mchezo wa netiboli timu mahiri ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma wameshika nafasi ya tatu baada ya kuwachapa bila huruma timu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa magoli 71-19, hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa magoli 33-7.
Katika mchezo wa mpira wa miguu timu ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU), waliwafunga Wizara ya Katiba na Sheria kwa magoli 4-2, ambapo katika dakika za kawaida walitoka sare ya bao 1-1 na ndipo sheria ya penati ikafuata na TAKUKURU wakashinda 3-1.
Katika hatua nyingine michezo ya fainali ya michuano hii inatarajia kufanyika kesho tarehe 15 Septemba kwa michezo ya kuvuta kamba wanawake na wanaume, mpira wa miguu na netiboli.
Michezo ya hii ya 39 ya SHIMIWI iliyoanza tarehe 01 Septemba, 2025 inatarajia kuhitimishwa Septemba 16, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...