Na Diana Byera,Bukoba

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imelifungua Ziwa Ikimba lililopo Halmashauri ya Bukoba, mkoani Kagera, ikiwa ni miezi 6 tangu lilipofungwa kwa lengo la kuongeza kiwango cha samaki kwenye ziwa hilo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kufungua ziwa hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa, amewataka wananchi wanaonufaika na uvuvi wa ziwa hilo kutoacha shughuli zilizokuwa zikiwaingizia kipato wakati ziwa lilipokuwa limefungwa ili kuwa na uchumi jumuishi kwenye eneo hilo.

“Niwapongeze sana kwa kutii makubaliano ya kutofanya shughuli za uvuvi katika kipindi chote cha ufungaji wa ziwa na leo sote tumeshuhudia matunda ya uvumilivu wenu kwa kipindi cha miezi 6. Niombe muendelee kutunza ziwa hili lakini tusiache shughuli nyingine pia tufanye shughuli zote ili kuinua uchumi wetu kwa vyanzo tofauti tofauti,” alisema Erasto.

Alisema kuwa ufunguzi wa ziwa hilo utaongeza mapato ya Halmashauri, ambapo mpaka sasa takribani shilingi milioni 8 zimeshapatikana kupitia usajili wa mitumbwi ya kuvulia samaki pekee. Pia alibainisha kuwa tani 15 kwa mwaka zitaongeza mapato makubwa ya Halmashauri hiyo na akashauri wavuvi waweke utaratibu wa kulipumzisha ziwa hilo mara kwa mara ili kuongeza samaki.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede, amesema kuwa wizara itaendelea kuchagiza shughuli za uvuvi kwenye ziwa hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya uvuvi unaokubalika kisheria na kuongeza takribani vifaranga milioni 1 vya samaki kabla ya mwisho wa mwezi Oktoba mwaka huu.

“Wataalam wetu wa wizara wataweka kambi hapa kwa ajili ya kutoa elimu hiyo lakini pia watakaa na ninyi darasani kabisa ili kuelimishana kuhusu uvuvi unaofaa na tutaongeza tena vifaranga katika ziwa hili,” alisema Dkt. Mhede.

Akielezea hali ya upatikanaji wa samaki ilivyo hivi sasa kwenye ziwa hilo, Mkurugenzi wa Uvuvi nchini, Prof. Mohammed Sheikh, alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa kitaalam uliofanyika leo ziwani hapo, kiwango cha mavuno ya samaki kwa mwaka kinatarajiwa kupanda kutoka tani 1.5 hadi kufikia tani 15, huku kiwango hicho kikitarajiwa kuongezeka zaidi endapo rasilimali za uvuvi zilizowekwa ziwani humo zitalindwa kikamilifu.

“Huu ni mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba uzalishaji unaongezeka, wananchi wanapata tija na mapato ya Serikali kupitia sekta ya uvuvi yanaongezeka,” alisema Prof. Sheikh.

Wavuvi wanaonufaika na ziwa hilo, Enickson Charles na Rehema Hamza, wamesema kuwa kufunguliwa kwa ziwa hilo na kiwango cha samaki wanaopatikana ni fursa ya wao kukuza uchumi wao kupitia maji hayo. Wameongeza kuwa watahakikisha wanalinda rasilimali hizo ili zisitoweke tena kama ilivyokuwa awali.

Ziwa hilo lilifungwa Machi 12, 2025 kwa makubaliano ya hiari baina ya Serikali, wavuvi na wananchi wanaonufaika na ziwa hilo kwa lengo la kuongeza kiwango cha uzalishaji wa samaki ili kukuza uchumi wa wakazi wa eneo hilo, mkoa wa Kagera na taifa kwa ujumla.








Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...