Na Pamela Mollel, Moshi
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Moshi Mjini kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi, huku mgombea wa ubunge wa jimbo hilo, Ibrahimu Shayo, akiweka wazi ajenda na dira yake ya kuibadilisha Moshi kuwa miongoni mwa majimbo bora zaidi nchini.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza, Shayo aliwaomba kumpa ridhaa ya kuwatumikia ili aweze kutekeleza ahadi alizozibainisha, akisema kuwa anataka kuifanya Moshi kuwa mfano wa majimbo mengine na kwamba kwa kushirikiana na wananchi, mji huo unaweza kubadilika.
Katika hotuba yake, Shayo alisema changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa Moshi kwa sasa ni tatizo la taka ngumu, ambapo magari ya kubebea taka yamechoka na hayatoi huduma kwa wakati. Alisisitiza kuwa akipewa ridhaa ya kuwa mbunge, atahakikisha usafi wa mji unakuwa wa mfano na taka hazitasumbua tena wananchi
Aidha, Shayo aliahidi kushughulikia tatizo la miundombinu ya barabara, akisema barabara nyingi zimeharibika vibaya na hazisaidii wananchi wala kuchochea maendeleo. Aliahidi kwamba kupitia nafasi ya ubunge atahakikisha barabara zinakarabatiwa na kujengwa mpya ili kuchochea uchumi wa wananchi.
Mbali na hayo, Shayo alizungumzia pia sekta ya viwanda, akisema Moshi imebarikiwa kwa kuwa na mazao mengi ya matunda lakini haina viwanda vya kuchakata Aliahidi kufufua viwanda vilivyokufa na kusimamia ujenzi wa vipya ili kuhakikisha mji huo unakuwa kitovu cha viwanda vya matunda na vijana wanapata ajira.
Kwa upande wake, kada maarufu wa CCM, Namelok Sokoine, aliwataka wanachama na wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi na kuhakikisha wanatoa kura za kishindo kwa wagombea wote wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na hadi urais.
Kampeni hizo zilipambwa na shamrashamra mbalimbali huku wananchi wakionesha hamasa kubwa na kumshangilia Shayo kwa shangwe, ishara ya kumuunga mkono katika safari yake ya kuelekea bungeni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...