Songea _ Ruvuma.

Jumla ya wanafunzi 223 wa kidato cha tano kutoka shule ya Sekondari Ruhuwiko, inayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi  Tanzania (JWTZ), wamehitimu mafunzo ya ukakamavu yaliyodumu kwa miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba 26, 2025.

Akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo iliyoandaliwa shuleni hapo Kamanda wa Brigedi ya Kusini Meja Jenerali Charles Peter Feruzi aliwataka wanafunzi na walimu wa shule hiyo kutimiza wajibu wao katika mapambano ya kielimu kwa lengo la kulea kizazi chenye elimu, uzalendo na maarifa yatakayosaidia kuijenga nchi.

Meja Jenerali Feruzi alisema kuwa juhudi zinazofanywa na walimu pamoja na walezi wa shule hiyo zina mchango mkubwa katika maandalizi ya viongozi wa baadaye, akisisitiza kuwa wanafunzi wanaolelewa sasa ndiyo msingi wa Taifa la kesho.

Aliongeza kuwa mafanikio ya wanafunzi hayapaswi kuangaliwa kwa kuzingatia mazingira tu, bali kwa kile wanachokizalisha kupitia mafunzo na elimu wanayopata.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Luteni Kanali Benedicto Simon Bahame, alisema kuwa mafunzo ya ukakamavu (Kwata) ambayo yamekuwa yakitolewa kwa wanafunzi wa shule hiyo kila mwaka yameleta matokeo chanya, hususani katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi. 

Alieleza kuwa kwa mwaka huu, shule hiyo imefanikiwa kutoa wanafunzi 274 wa kidato cha sita waliokuwa wakifanya mtihani wa mwisho, ambapo wanafunzi 185 walipata daraja la kwanza, 87 daraja la pili na wawili tu walipata daraja la tatu.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kijeshi na Kiraia, walimu,  pamoja na wanafunzi wa shule hiyo. Wanafunzi wote 223 waliomaliza mafunzo ya ukakamavu walitunukiwa vyeti vya pongezi na Kamanda Brigedi Meja Jenerali Charles Peter Feruzi, ikiwa ni ishara ya kutambua juhudi na kujituma kwao katika kipindi chote cha mafunzo.

Mafunzo ya ukakamavu hufanyika kila mwaka kwa wanafunzi wa kidato cha tano katika shule ya sekondari Ruhuwiko kama sehemu ya maandalizi ya kuwaimarisha kiakili, kimwili na kinidhamu.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...