Songea_Ruvuma.
Meneja Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), Jumanne Gayo, amesema zaidi ya wateja 1,000 kati ya 2,000 waliokuwa wamesitishiwa huduma ya maji kutokana na madeni, tayari wameunganishwa tena na huduma hiyo kupitia ofa maalum ya urejeshaji huduma iliyoanza Agosti 4, 2025.
Akizungumza leo Septemba 4, 2025, Gayo amesema ofa hiyo ya miezi miwili inayotarajiwa kumalizika Oktoba 4, 2025 imepokelewa kwa mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi, hali inayoashiria uelewa unaoongezeka kuhusu umuhimu wa kurejesha huduma ya maji safi majumbani.
“Tunawashukuru wananchi kwa kuitikia wito wetu, Kupitia ofa hii, hakuna faini yoyote inayotozwa kwa wateja waliositishiwa huduma. wanachotakiwa kufanya ni kulipa deni lao tu na huduma inarejeshwa mara moja ndani ya masaa 24” amesema Gayo.
Aidha, amewasihi wateja kuhakikisha wanakagua mara kwa mara miundombinu ya maji majumbani mwao ili kuepuka malalamiko ya bili kuwa kubwa, akisisitiza kuwa ukusanyaji wa mapato ndio msingi wa uendeshaji wa shughuli za Mamlaka.
Kwa upande wake, Mhandisi Vicent Bahemana kutoka SOUWASA, amewakumbusha wateja kuwa kila tone la maji lina thamani na linapaswa kulipiwa, amehimiza ulinzi wa miundombinu ya maji kwa kuhakikisha hakuna mivujo inayopoteza maji na kusababisha gharama kubwa kwa wateja.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Manispaa ya Songea, Mhandisi Bahemana amesema kufikia Agosti 2025, kiwango cha usambazaji maji kimefikia asilimia 94, huku lengo la Mamlaka likiwa ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwaka 2030.
Naye Afisa Uhusiano na Mawasiliano kwa Umma wa SOUWASA, Juma Mwakaje, amesema Mamlaka inaendelea na kampeni ya kutoa elimu kwa wananchi kwa kutembelea nyumba kwa nyumba ili kubaini changamoto zinazowakwamisha wateja kurejesha huduma pamoja na kuhamasisha ushirikiano wa jamii katika kubaini maunganisho haramu ya maji.
“Tunawaomba wateja wetu waendelee kushirikiana nasi, zoezi hili litasaidia kuboresha huduma na kukomesha vitendo vya kuhujumu miundombinu ya maji,” amesema Mwakaje.
SOUWASA inatoa wito kwa wateja wote waliositishiwa huduma ya maji kutumia kikamilifu kipindi hiki cha ofa maalum, ili waondokane na adha ya kutafuta maji kwa majirani na kuipata huduma kwa urahisi, bila gharama za ziada.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...