SONGEA_RUVUMA.
Maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa Mkoa wa Ruvuma yamefanyika leo katika Uwanja wa Majimaji Mjini Songea, yakiongozwa na Afya Club Ruvuma kwa kushirikisha na wananchi, viongozi mbalimbali, pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Jumanne Mwankoo, amewataka wananchi kuzingatia mazoezi ya mwili kwa ajili ya kuimarisha afya, akibainisha kuwa afya bora ni msingi wa maendeleo ya taifa.
Amesema hayati Mwalimu Nyerere aliwahi kufafanua juu ya maadui wakuu wa taifa ambao ni maradhi, ujinga na umasikini, hivyo jitihada zote zinazofanyika leo zinaendeleza mapambano dhidi ya maadui hao kwa mujibu wa falsafa yake.
Katika sekta ya afya, Mwankoo amesema serikali imeendelea kujenga hospitali kuanzia ngazi ya vijiji hadi mikoa ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, Aidha kwa upande wa elimu, shule za sekondari na msingi zimejengwa kila kata, na katika nyanja ya uchumi, Tanzania imepiga hatua kwa kufikia uchumi wa kati yote ikiwa ni ishara ya utekelezaji wa dira ya Mwalimu Nyerere.
Kauli mbiu ya mwaka huu imebeba ujumbe wa kitaifa unaosema “Tumuenzi Baba wa Taifa kwa kushiriki Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kwa amani na utulivu.”
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Louis Chomboko, amesema Oktoba 14 ni siku muhimu ya kutafakari kwa pamoja fikra, amani, utu na umoja aliouacha Mwalimu Nyerere, amesisitiza kuwa njia bora ya kumuenzi Baba wa Taifa ni kwa vitendo na si kwa maneno, kwa kuendeleza falsafa zake za upendo, mshikamano na haki kwa wote.
Mapema leo asubuhi, wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama walifanya jogging kama ishara ya kuimarisha afya na ustawi wa jamii, Washiriki walishuhudia pia michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu na mpira wa pete katika viwanja hivyo.
Afya Club Ruvuma imeendelea kuonyesha mfano wa kuigwa katika maadhimisho hayo kwa kuanza shughuli zake Oktoba 13 kupitia maandamano kutoka ofisi ya Mkuu wa Wilaya hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa ajili ya kufanya usafi, na kisha kuelekea Soko Kuu la Songea kwa usafi wa mazingira pamoja na zoezi la upimaji wa afya kwa wananchi.
Maadhimisho ya mwaka huu pia yamelenga kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 kwa amani, utulivu na mshikamano msingi mkuu ulioasisiwa na Baba wa Taifa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...