*Pia aweka wazi mkakati kufufua viwanda vya Ginery kuongeza thamani ya pamba

Na Said Mwishehe,Michuzi TV

MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wananchi mkoani Mwanza Serikali katika miaka mitano ijayo  itaendelea na ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya usafiri ikiwemo kukamilisha ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kati ya Mwanza na Dar es Salaam.

Mradi ambao ukikamilika utafungua uchumi wa Tanzania kutokana na miji hiyo miwili yenye uchumi mkubwa nchini kupungua saa za kusafirisha bidhaa na abiria huku akifafanua kutoka Mwanza hadi Dar es Salaam kwa kutumia treni ya SGR ni saa 8 wakati kwa sasa usafiri wa basi ni kati ya saa 18 hadi saa 20.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Nyamagana Mjini Mwanza mbele ya maelfu ya wananchi Dk.Samia amesema mradi wa ujenzi wa SGR kwa sasa upo katika hatua za kati kukamilisha kipande cha Mwanza hadi Isaka umbali wa kilomita 314, ambapo utagharimu fedha Sh.trilioni 3 ujenzi na ujenzi umefikia asilimia 63.

" SGR kati ya Mwanza na Isaka utakuwa na stesheni tano ambazo zitainua shughuli za kiuchumi za mkoa huo.Pia tutajenga maghala ya kuhifadhia bidhaa kwa ajili ya kusafirialdha mizigo. Ni muhimu kwa fursa za ajira."

Akifafanua zaidi Dk.Samia amesema pia pale Fela kuna Bandari Kavu itakayotumika kupakia na kupakua mizigo na kuongeza hivi sasa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma mambo safi.

"Kuna watu wanasafiri kwa ajili ya vikao wanarejea siku hiyo hiyo; reli hii ina manufaa makubwa sana," amesema  Dk. Samia na kuongeza "Baada ya kuunganika reli kati ya Mwanza hadi Dar es Salaam itapunguza umbali wa safari kutoka saa 20 hadi saa nane pekee."

Mgombea urais Dk.Samia ambaye katika mkoa wa Mwanza ametekeleza miradi mbalimbali amesema itakapokamilika reli ya SGR itarahisisha biashara kati ya Mwanza na Dar es Salaam.

"Kuna watu ambao kwa sasa analazimika kusubiri mzigo wake kwa siku mbili,lakini kwa kutumia SGR atasafirisha mzigo na kuupata siku hiyo hiyo."

Hivyo ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu wahakikishe wanaicuagua CCM ili ipate ridhaa ya kuongoza nchi na kazi kubwa itakuwa ni kukamilisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa reli hiyo ya SGR.

Wakati huo huo Dk.Samia ameeleza Kanda ya Ziwa ni maarufu kwa kilimo cha Pamba hivyo ahadi ya Serikali katika miaka mitano ijayo itahakikishia inafufi viwanda vya Ginery ambavyo ni maalum kwa kuchakata pamba ili kuiongezea thamani hasa kwa kuzingatia pamba hiyo inatumika kutengeneza shuka,nyuzi na pamba za hospitali.

"Tutafufua viwanda vya Ginery vya Sengerema, Buchosa na Manawa ili  tuzalishe bidhaa za Pamba kwa wingi, kuna vitu vingi tunaagiza nje hasa sekta ya afya kama Pamba za kusafisha vidonda, Bendeji na vitu vingine kama shuka tunatumia fedha za kigeni kuagiza wakat Pamba tunazalisha nchini." Amesema Dk.Samia.

Hata hivyo amesema Serikali inasambaza mbegu za pamba na dawa bure bila malipo huku pia akiahidi kusambaza vijana 700 kwa ajili ya huduma za ugani ili kuongeza uzalishaji. 

"Tayari tumeshaagiza trekta 700 na kati hizo treka 350 zimeshafika tutazisambaza kwa ajili ya kulima kwa nusu bei. Tutayasambaza kwenye vituo vya zana za kilimo sio kwa Mwanza tu bali kote nchini."

Akieleza zaidi amesema pia mpango wa Serikali baada ya kukamilisha mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria itatumia njia hizo hizo za kusafirisha maji ili kufanya miradi ya umwagiliaji.

Amesema kuwa nchini kuna maziwa yenye maji mengi na ya kutosha kwa shughuli mbalimbali lakini maji hayo hayajatumika ipasavyo hivyo mpango wa Serikali ni kuhakikisha maji ya ziwa Victoria yanatumika kwa kilimo cha umwagiliaji.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...