*Azungumzia kuhusu ujenzi bandari ya Kalema na ujenzi wa meli

*Pia aelezea mkakati ujenzi reli kutoka Kaulia ,agusia usafiri wa anga


Na Said MwisheheMichuzi TV-Rukwa

MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amefanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Mji wa Mpanda mkoani Katavi ambapo amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika mkoa huo kwa kufungua njia za barabara, anga, reli na majini pamoja na kuwezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Azimio uliopo Mpanda Mjini mkoani Katavi ,Mgombea Urais Dk.Samia amesema katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, serikali imekamilisha ujenzi wa Bandari ya Kalema iliyopo mwambao wa Ziwa Tanganyika.

Amefafanua ujenzi wa bandari hiyo umegharimu fedha Sh.bilioni 47.9 na kwamba utarahisisha usafirishaji abiria na mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi na Zambia.

Mgombea urais Dk.Samia amesema ujenzi wa bandari unaenda sambamba na ujenzi wa meli nne za mizigo katika Ziwa Tanganyika huku akieleza pia Serikali imeweka lengo hadi kufikia mwaka 2030 mizigo inayotoka Tanzania kwenda Congo iwe inapita katika bandari hiyo.

Akieleza zaidi amesema  kwamba bandari na reli zinategemea hivyo serikali imeshafanya usanifu kufanya maboresho reli ya Kaliua - Mpanda yenye urefu wa kilometa 210.

Alieleza kuwa maboresho hayo yatapunguza muda wa usafirishaji mizigo kwa njia ya reli kutoka kati ya saa saba hadi nane na sasa kufikia saa mbili hadi tatu.

Wakati huo huo amesema Serikali imeimarisha usafiri wa anga kwa kukarabati uwanja wa ndege Mpanda ikiwemo ujenzi wa jengo la abiria.Uimarishaji huo umewezesha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kufanya safari za Dar es Salaam - Mpanda mara tatu kwa wiki.“Hatua hiyo imesaidia kuimarisha biashara na shughuli mbalimbali za maendeleo.”

Kuhusu barabara, Dk.Samia amesema barabara muhimu inayounganisha Wilaya ya Tanganyika (Katavi) na Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma imeanza kuijenga kwa kiwango cha lami.

“Barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 250.4 inajengwa kwa vipande vinne, hivyo aliwaahidi wananchi kwamba serikali itaendelea na kasi kukamilisha mradi huo.”

Hata hivyo amewahakikishia wananchi kuwa barabara ya Mpanda - Ugala - Kaliua itakuwa miongoni mwa vipaumbele vya ujenzi katika mkoa huo huku akisisitiza kuna barabara zilizoandikwa kwenye ilani ya uchaguzi ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami na cha changalawe.

Dk.Samia pia amesema kuna uhitaji wa madaraja katika maeneo muhimu ambayo yanaendana na ujenzi wa barabarani na kwamba Katika miaka mitano ijayo Serikali inakwenda kujenga daraja la Kakese - Itenka pamoja na madaraja madogo.

Kuhusu madai ya fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo ambapo wapo wananchi 250 waliopisha ujenzi wa barabara Mpanda - Sikonge amesema wapo wananchi 830 waliopisha ujenzi wa barabara Mpanda - Sitalike, aliwaahidi ataielekeza Wizara ya Ujenzi kufanya upembuzi wa madai hayo.

Akizungumzia huduma za mawasiliano, Mgombea Dk.Samia amesema mkoa huo una minara 64 ambapo 63 imekamilika na kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi.

Pia amesema katika kilimo Serikali imefanya uwekezaji mkubwa ili kuzidisha uzalishaji wa mazao ya kilimo mara dufu na kuahidi itaendelea kutoa ruzuku, kujenga skimu za umwagiliaji na maghala kuufanya mkoa huo kuendelea kuzalisha mazao kwa kiasi kikubwa.

Aidha amesema Serikali ilijenga vituo vinne vya kukusanya na kuchakata mazao ya nyuki.”Nampongeza Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda kwa kuhamasisha uzalishaji asali hivyo kupitia sekta ya misitu, uzalishaji asali umewekwa katika mpango wa Jenga Kesho Iliyobora (BBT).”

Wakati katika  mipango ya sekta ya uvuvi ni pamoja na kujenga mabwawa, vizimba na vituo vya ukuzaji viumbemaji Ziwa Tanganyika.

Ametumia mkutano huo kutoa rai  kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo ili waweze kujiajiri na kuajiriwa kupitia ufugaji samaki.

Pia amesema Serikali itajenga soko la mazao Kata ya Mpanda hoteli huku akiahidi serikali kujenga machinjio ya kisasa ya mifugo.

“Serikali inajipanga katika kila wilaya kuanzisha kongani za viwanda baada ya kufikisha huduma ya umeme katika vijiji na vitongoji.Viwanda hivyo vitaongeza thamani mazao katika mkoa huo hali itakayoongeza wigo wa masoko ya ndani na kimataifa.”

Dk.Samia amesema Serikali katika miaka mitano iliyopita imeanza na viwanda vikubwa vitano na vyakati 20 ndani ya mkoa huu. Jumla ya ajira 5,828 zimepatikana kupitia viwanda hivyo.

Kwa upande wa sekta ya afya serikali imejenga hospitali za rufaa, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati.”Katika miaka mitano ijayo Serikali inakwenda kuongeza kasi ya ujenzi wa hospitali na vituo vya afya.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...