FARIDA MANGUBE MOROGORO


Mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuathiri kwa kiwango kikubwa ustawi wa jamii na mazingira hali inayoongeza haja ya elimu na uelewa wa pamoja kama silaha kuu ya kupambana na changamoto hiyo.

Akifunga Kongamano la Pili la Kisayansi la Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano lililofanyika mjini Morogoro, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala, amewataka wananchi kuachana na vitendo vya uharibifu wa mazingira ikiwemo uchomaji moto misituni, uharibifu wa vyanzo vya maji na uvamizi wa maeneo yasiyostahili shughuli za kibinadamu.

“Msingi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ni elimu. Jamii nzima inapaswa kushirikiana katika kuelimisha wananchi ili wajue athari za vitendo vyao kwa mazingira, kwa kuwa jukumu la kulinda mazingira si la Serikali pekee, bali ni la kila mmoja wetu,” alisema Kilakala.

Kwa upande wake, Prof. Japhet Kashaigili, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uzamili, Utafiti, Uhaulishaji wa Teknolojia na Ushauri wa Kitaalamu na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya kongamano hilo, amesema kikao hicho kimeazimia hatua muhimu za utekelezaji ikiwemo kuendeleza programu za ubadilishanaji wa wanafunzi na walimu ili kujenga uwezo wa pamoja.

Pia kuanzisha vituo vya teknolojia na ubunifu, kuandika maandiko ya pamoja ya utafiti yenye suluhu kwa changamoto za jamii na kuchambua masuala ya kisera na kuyawasilisha serikalini, hususai katika sekta za afya, maji na mabadiliko ya tabianchi, ili kusaidia Serikali kuunda sera shirikishi zinazotokana na tafiti za kitaalamu.

Naye Dkt. Safiness Simon Msollo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka SUA, amesema kongamano hilo limetoa mwanga mkubwa juu ya umuhimu wa kuunganisha matokeo ya tafiti na jamii. Huku akisisitiza  kuwa tafiti hazipaswi kubaki maktabani pekee, bali lazima ziwe endelevu na zenye mchango wa moja kwa moja kwa wananchi.

Kongamano lijalo la Tatu la Kisayansi la Muungano wa Vyuo Vikuu Vitano limepangwa kufanyika katika Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST) jijini Arusha.


 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...