Farida Mangube, Morogoro

Shiriki la kimataifa lisilo la Kiserikali la Islands of Peace Tanzania wameeleza mpango wa kuongoza mageuzi makubwa kwenye sekta ya Kilimo kwa kuviwezesha vituo mbalimbali vinavyotumika kutoa mafunzo ya mbinu bora za kilimo kwa wakulima kupitia mradi wake wa AGRO KILIMO uliopangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili.

Akizindua mradi huo, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Anne-Sophie Avé, alisema mataifa hayo mawili yamekuwa washirika wa karibu katika sekta za kilimo ikolojia na elimu kwa miaka mingi, jambo lililoleta matokeo chanya katika kukuza teknolojia na kuendeleza kilimo kinachoangazia uhifadhi wa mazingira.

Mradi huo unaojulikana kama AGRO KILIMO, unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili kwa kushirikiana na vituo sita vya mafunzo ya kilimo vilivyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia vituo hivyo, wakulima na vijana watapatiwa mafunzo ya vitendo juu ya mbinu bora na bunifu za kilimo, hususan zinazolenga kuimarisha usalama wa chakula na kujenga mifumo endelevu ya kilimo.

Mkurugenzi wa Islands of Peace Tanzania, Ayesiga Buberwa, alisema mradi huo utaimarisha mashamba darasa na kuyawezesha kuwa kitovu cha maarifa na vitendo.

Pia vituo vya mafunzo vitapatiwa msaada kulingana na mahitaji yao, ikiwemo miundombinu na elimu kwa watendaji, huku Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kikihusishwa moja kwa moja katika tafiti na utekelezaji.

“Tumedhamiria kuviwezesha vituo hivi kujifunza pia nje ya Tanzania. Dunia sasa ni kijiji, hatuwezi kubaki eneo moja. Mradi utawajengea uwezo watendaji na kuviunganisha vituo na SUA hususan katika utafiti,” alisema Buberwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Mitaala na Utafiti kutoka Wizara ya Kilimo, Dkt. Mashaka Mdangi, alisema mradi huo umejikita kwenye vipaumbele vya serikali, ikiwemo kuongeza tija ya mazao ya chakula na biashara, kueneza mbinu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na kusambaza maarifa ya kilimo-ikolojia kwa wakulima wengi zaidi.

Uzinduzi huo uliofanyika mkoani Morogoro ulihudhuriwa na viongozi wa serikali, wawakilishi wa SUA, wadau wa maendeleo na viongozi wa vituo vya mafunzo ya kilimo, ambapo wote walisisitiza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Ufaransa utasaidia kulinda mustakabali wa kilimo na mazingira nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...