Mgombea Ubunge Jimbo la Peramiho ambaye  ni Waziri wa Afya Jenista Mhagama, ameendelea na kampeni zake leo Oktoba 11, 2025, katika Kata ya Maposeni Kijiji cha Mdundualo, akiwaomba wananchi kuichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29.

Katika mkutano huo wa kampeni, Mhagama alisisitiza kuwa kampeni za mwaka huu ni za kuimarisha mafanikio yaliyopatikana kupitia ahadi zilizotolewa katika uchaguzi uliopita, alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imetekeleza kwa mafanikio makubwa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati, upatikanaji wa huduma za maji na usambazaji wa umeme hadi kwenye vijiji.

Akizungumzia historia ya ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho, Mhagama alibainisha kuwa awali zilitolewa saruji ambazo hadi ziliganda kutokana na kukwama kwa utekelezaji wa mradi, lakini hali hiyo imebadilika baada ya Serikali ya Awamu ya Sita kupeleka fedha na kukamilisha ujenzi huo kwa mafanikio.

Sekta ya nishati pia imepiga hatua, ambapo alisema umeme umefika katika ngazi ya vijiji na kilichobaki ni kukamilisha usambazaji kwenye vitongoji vichache vilivyosalia, alisisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kuendelezwa endapo wananchi hawatatiki kwa CCM katika uchaguzi huu.

Mhagama alieleza kuwa Serikali ya CCM imeweza kupeleka mbolea ya ruzuku, maji safi, huduma za afya na elimu, na kusisitiza kuwa baada ya uchaguzi mafanikio hayo yataongezeka zaidi, Alimtaja Rais Samia Suluhu Hassan kuwa kiongozi mwenye maono ambaye amedhihirisha uwezo mkubwa wa kuwatumikia Watanzania.

Kuhusu ilani ya uchaguzi ijayo, alisema itazingatia mahitaji ya makundi maalum kama wazee, wajawazito na watoto kwa kuwapatia bima ya afya, Aliahidi kuwa ndani ya siku 100 za mwanzo baada ya uchaguzi, serikali itasimamia matibabu ya wananchi wasio na uwezo wa kugharamia huduma za afya, hasa kwa magonjwa makubwa.


Aidha, alibainisha kuwa baada ya kutatua changamoto nyingi, sasa CCM itajielekeza kwenye miradi ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa daraja, ukarabati wa barabara ya Peramiho–Maposeni ambayo tayari imetengewa shilingi milioni 100, na mpango wa kuunganisha Kijiji cha Litowa na Mdundualo.

Alitangaza pia kuwa Halmashauri ya Peramiho inapangwa kupandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji kupitia ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025–2030, hatua itakayowezesha upanuzi wa barabara za lami, zahanati, shule na huduma nyingine za kijamii.

Katika sekta ya kilimo, Mhagama alibainisha kuwa serikali itaanzisha mikopo maalum kwa wakulima na kuanzisha visima zaidi ya 150 kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji jatika jimbo hilo. Alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha wanachagua CCM ili wanufaike na miradi hiyo, huku akisisitiza kuwa wakulima watahamasishwa kuuza unga badala ya mahindi ili kuongeza thamani ya mazao.

Masuala ya migogoro ya ardhi na kati ya wakulima na wafugaji pia yamepewa kipaumbele, ambapo serikali ya CCM imejipanga kuyatatua kabla ya msimu mpya wa kilimo kuanza.

Kwa upande wa TASAF, aliahidi kuwa mpango huo utaendelea, pamoja na kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana, na kuhifadhi makumbusho ya historia ya mababu kama sehemu ya urithi wa taifa.

Katika mkutano huo, Sweetbert Shawa aliyewahi kuwa mtia nia wa udiwani Kata ya Maposeni, aliwaomba wananchi waendelee kuiamini CCM na kumpongeza Jenista Mhagama kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo, akisisitiza kuwa ni tunu ya kuendelezwa.

Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Songea Vijijini Thomas Masolwa, naye alihimiza wananchi kuhakikisha wanapiga kura kwa wagombea wa CCM katika nafasi za urais, ubunge na udiwani, kwa kuwa maendeleo yote yanayoonekana ni matokeo ya utekelezaji wa sera za chama hicho.

Mgombea udiwani Kata ya Maposeni, Monica Tambala, alieleza mafanikio yaliyopatikana awamu iliyopita likiwemo suala la maji, zahanati, barabara, umeme na ujenzi wa shule maalum kwa watoto. Alitoa wito kwa wananchi kuhakikisha CCM inapata ushindi kwenye ngazi zote.

Mkutano huo wa kampeni umefanyika katika Kijiji cha Mdundualo, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikutano ya kuomba ridhaa ya wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...