📌 Vijana watakiwa kuacha kutumika kuvuruga amani

MASHAKA MHANDO, Tanga

MKUU wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batlida Burian amewataka vijana nchini kuachana na shinikizo la watu wa kwenye mtandao wanaotaka kuvuruga amani ya nchi ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.

Akizungumza katika sherehe za kumbukumbu ya baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere iliyoambatana na maadhimisho ya 'Siku ya Chakula Duniani' inayofanyika Kitaifa Jijini Tanga, Mkuu wa mkoa alisema kuwa Amani ya nchi inatakiwa kusimamiwa kwa nguvu zote kwa kuzungumza na vijana waache wakutumika.

"Tuisimamie Amani kwa nguvu zetu zote tuongee na vijana wetu waachane na mambo ya watu wa kwenye mtandao, wanalipwa ili kuvuruga amani yetu, madhara yakitokea sisi tunaoishi nchini tutapata shida kuliko wao," alisema Balozi Burian.

Alisema vijana wanatakiwa kuwa Wazalendo wa nchi yao kama ambavyo Baba wa Taifa alifanya kwa kuwapeleka kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambako huko pamoja na kupata stadi za maisha lakini walifundishwa uzalendo wa nchi yao.

Alisema baba wa Taifa angekuwepo leo hii angewachapa bakora vijana wanao tumiwa na mabeberu wa nje kwa ajili ya kuvuruga amani ya nchi hatua ambayo alisema wakati huu wa kumbukumbu ya Mwalimu ni vema wazazi wakawakumbusha vijana wajibu wa kuilinda Tanzania.

Hata hivyo, Mkuu wa mkoa huyo alimpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufuata yake mema ambayo aliusia hayati baba wa Taifa ikiwemo kupiga vita maadui watatu Ujinga, maradhi na umasikini.

Alisema katika kupiga vita ujinga serikali ya awamu ya sita imejenga shule nyingi nchini lakini pia imejenga hospitali, vituo vya afya pamoja na kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa wananchi ili kuondoa umasikini wa kipato.

Awali Mkuu wa wilaya ya Tanga Dady Kolimba alisema kuwa hayati baba wa Taifa alikuwa kiongozi wa kipekee duniani aliyekuwa kiongozi kwa muda mrefu kisha akaacha madaraka hayo mwenyewe licha ya kukaa miaka mingi.

Kolimba alisema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na sifa nyingi ikiwemo kukumbukwa kwa sera zake za kujali utu kwa kuanzisha azimio la Arusha ili kuondoa matabaka ya aliyekuwa nacho na asiyekuwa nacho.

"Nyerere alikuwa mwanaharakati aliyepigania uhuru wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika, lakini pia ni mtu pekee aliyeandikwa kwenye historia kwa kuweza kuwaunganisha Watanzania zaidi ya makabila 120 kuwa wamoja kwa kuzungumza kiswahili," alisema Kolimba.

Alisema katika falsafa ya Mwalimu ya kuondoa ujinga, maradhi na umasikini Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ameitendea haki wilaya ya Tanga kwa kujenga madarasa 312 na kulipa shilingi bilioni 4.96 kwa ajili ya kugharamia elimu bure.

Kwa upande wa afya alisema Rais amejenga hospitali ya wilaya ya Tanga, kujenga vituo vya afya, zahanati na nyumba za watumishi katika sekta ya afya hatua ambayo imeweza kusaidia kusogea huduma karibu na wananchi.

"Kwa upande wa faslafa ya umasikini Rais Samia ametoa mikopo ya jumla ya shilingi bilioni 4.46 kwa wajasiriamali wa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, " alisema Dady.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Charles Kalagi mwakilishi mkazi wa Shirika la chakula Duniani (FAO), Martine Sipanjo Mkurugenzi wa huduma za Copra na washiriki wengine wakiwemo wazee wa Tanga ambao walimwelezea Mwalimu Nyerere wakati wa uhai kazi zake na maono aliyokuwa nayo.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...