Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kupitia Mradi wa kujenga uwezo katika Usimamizi wa Utekelezaji wa Sheria ya Mazingira (EMA), limeanza kutoa mafunzo kwa maafisa forodha waliopo mipakani, taasisi, wizara, idara pamoja na vyombo vya serikali kuhusu usimamizi wa bidhaa hatarishi kwa mazingira zinazopita mipakani.

Mafunzo hayo yamezinduliwa Oktoba 15, 2025 katika ofisi za Forodha Mtukula na yanatarajiwa kufanyika katika mipaka ya Rusumo, Kigoma na Tunduma kwa lengo la kuimarisha uelewa na uwezo wa watendaji wa serikali katika kusimamia utekelezaji wa Sheria na taratibu za mazingira kwa bidhaa zinazoingia na kutoka nchini.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi huo, Bw. Paul Kalokola ambaye pia ni Afisa Mazingira Mkuu wa NEMC, amewataka washiriki kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Sheria za mazingira na kuhakikisha bidhaa zote zinazovuka mipaka zinakidhi matakwa ya kisheria.

“Ni wajibu wa maafisa wote wanaohusika na usimamizi wa mipaka kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia au kutoka nchini hazina athari hasi kwa mazingira. Utekelezaji sahihi wa Sheria na Kanuni za mazingira utasaidia kulinda afya za wananchi na kudhibiti taka hatarishi zinazoweza kuathiri mfumo wa ikolojia,” alisema Bw. Kalokola.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Mfawidhi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) – Mtukula, Bw. Elpidius Bigilwamungu, ameishukuru NEMC kwa kutoa mafunzo hayo muhimu, akisisitiza kuwa elimu hiyo itasaidia kuongeza ufanisi katika utambuzi na udhibiti wa bidhaa hatarishi mipakani.

Katika mafunzo hayo, wataalamu kutoka NEMC wamewasilisha mada mbalimbali zikiwemo Tathmini ya Athari kwa Mazingira, Mwongozo wa Utoaji wa Vibali vya Kudhibiti Taka Hatarishi, Mikataba na Miongozo ya Kimataifa ya Usimamizi wa Mazingira, Masuala ya Sera za Mazingira pamoja na Matumizi Salama ya Zebaki.

Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi endelevu za Serikali kupitia NEMC na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) katika kuhakikisha utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) unafanyika kwa weledi, ushirikiano na uwajibikaji, hasa katika maeneo ya mipakani ambayo ni lango kuu la bidhaa kuingia nchini.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...