MKAGUZI wa Polisi kutoka Kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Mtandao, PF 22863 John Kaaya (45), ameieleza Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, namna alivyogundua maudhui yenye viashiria vya jinai katika picha mjongeo (video clip) alipokuwa akifanya doria mtandaoni.
Kaaya ametoa ushahidi huo leo Oktoba 9,2024 katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, likisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema, Kaaya amesema yeye ni mpelelezi katika dawati la doria mtandaoni, akifafanua kuwa kazi yake ni kufuatilia maudhui katika mitandao mbalimbali ya kijamii kama YouTube, Instagram, TikTok, Facebook na mingineyo.
Ameeleza kuwa doria hizo hufanyika saa 24 kila siku, kwa siku saba za wiki, kwa mfumo wa zamu unaopangwa ofisini, na lengo kuu ni kubaini makosa ya jinai yanayofanywa kupitia mitandao, kwa kutumia programu maalum za uchunguzi wa kidijitali.
Shahidi huyo amesema kuwaAprili 4, 2025, akiwa zamu kuanzia saa 12:00 asubuhi, alianza kukagua kompyuta yake ya kazi na kujiridhisha kuwa ipo salama kwa matumizi. Baadaye aliingia katika mtandao wa YouTube na kufika kwenye ukurasa wa www.youtube.com/@JamboTv,
ambapo aliona video yenye kichwa cha habari “Tundu Lissu uso kwa uso na wafuasi wa CHADEMA Majimboni: No Reform No Election – Njia Panda.”
Kaaya ameeleza kuwa alivutiwa kuchunguza video hiyo kutokana na idadi kubwa ya watazamaji na maoni yaliyokuwa yakitolewa, na alipoiangalia alibaini maudhui yenye viashiria vya jinai.
Kwa mujibu wa ushahidi wake, video hiyo ilimuonyesha Lissu akizungumza maneno yafuatayo
“Na ninyi mnataka mteuliwe kwenye cheo fulani? Nchi hii kwa hali ilivyo, hili linawezekana? Kama haliwezekani tufanyaje? Mkutano wetu unasema No Reforms, No Election. Wamesema kitu kimoja sahihi hapo. Msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli, ni kweli kwa sababu tumesema tutazuia uchaguzi, tutakinukisha sana sana.”
Baada ya kugundua hilo, Kaaya amesema alimjulisha Mkuu wake wa Kitengo ambaye alimuelekeza kuonana na Naibu Kamanda wa Upelelezi Kanda Maalum Dar es Salaam (ACP) George Bagyemu.
Kaaya ameeleza kuwa alipofika kwa ACP Bagyemu na kutoa maelezo kuhusu video hiyo, alipewa maelekezo ya kuandaa taarifa rasmi. Kisha mnamo Aprili 7, 2025, alirudi tena kwa ACP Bagyemu ambaye alimuelekeza kupakua video hiyo na kuihifadhi kwa mfumo maalum.
Shahidi huyo amesema alitumia flash disk mpya kupakua video hiyo kwa mfumo wa MP4, ikiwa na urefu wa saa tatu na ukubwa wa MB 500, zoezi ambalo lilichukua dakika 15 kukamilika. Ameeleza kuwa video hiyo aliambatanisha na fomu ya PF 145 kisha kuiwasilisha kwa ACP Bagyemu kama kielelezo DM, kwa ajili ya uchunguzi wa kitaalamu wa picha.
Ameongeza kuwa siku hiyo hiyo, ACP Bagyemu alimwita na kumtaka kumpatia nywila (password) aliyoitumia kulinda kielelezo hicho ili kuruhusu timu ya wachunguzi kuendelea na kazi.
Baada ya Kaaya kumaliza kutoa ushahidi wa awali, Wakili Mrema ameeleza kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa umekamilisha mahojiano yake na shahidi huyo. Lissu naye ameeleza kuwa yuko tayari kuanza maswali ya dodoso, lakini Mahakama ikaahirisha shauri hilo hadi kesho kwa kuendelea na usikilizwaji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...