Taasisi ya Watu Wenye Ulemavu nchini (TAJU) imewataka Watanzania wa ngazi zote kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, kwa kuzingatia amani, mshikamano na upendo ndani ya jamii.

Akizungumza kwenye hafla fupi ya kuombea amani uchaguzi jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TAJU, Ndonge Said Ndonge, amesema kuwa mara nyingine chaguzi zimekuwa chanzo cha vurugu na uvunjifu wa amani, siyo tu nchini Tanzania bali pia katika mataifa mengine.

"Kwa kutambua hili, TAJU kwa nia nzuri na ya kizalendo imeona ni lazima kuzungumzia jambo hili ili kuhakikisha nchi inabaki kuwa kisiwa cha amani na salama kwa kila Mtanzania, wakiwemo watu wenye ulemavu," amesema Ndonge.

Mwenyekiti huyo pia amebainisha kuwa mara nyingine dhana zinazojitokeza ni kwamba katika machafuko akina mama na watoto ndio wanaoathirika zaidi. Hata hivyo, TAJU imeeleza kuwa kundi la watu wenye ulemavu linaathirika kwa kiwango kikubwa lakini mara nyingi linasahaulika, hali inayofanya taasisi hiyo kulihimiza kundi hilo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa TAJU Taifa, Innocent Gabriel, amesema sauti za watu wenye ulemavu ni sehemu muhimu ya jamii na hivyo anatoa wito wa kushiriki kwa umoja na nguvu katika kumchagua viongozi watakaoiongoza nchi.

Emanuel Majeshi, Mratibu wa Dawati la Watu Wenye Ulemavu, amesema kuwa ili uchaguzi uwe wa haki na amani, ni muhimu viongozi na wasimamizi wa uchaguzi watende haki ili kila mshiriki aridhike na mchakato na matokeo ya uchaguzi.

Aidha, TAJU imetoa wito kwa washiriki wote wa uchaguzi, wakiwemo wagombea na vyama vya siasa, kuzingatia sheria zilizopo ili kuepuka vurugu na uvunjifu wa sheria. Viongozi wa dini pia wameombwa kushirikiana katika kuombea taifa kwa kufanya sala za maombi ya amani.

Kauli mbiu ya taasisi hiyo ya mwaka huu ni: "Tupange Wote, Tutekeleze Wote, na Tutathmini Wote", ikilenga kuhimiza mshikamano na ushirikiano katika kila jambo linalohusu maendeleo ya jamii ya Watanzania.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...