Afisa miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David akikagua maabara ya Sayansi Shule ya Sekondari Itumba ambayo imekarabatiwa na kumaliziwa ujenzi na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.

*******************

Na Mwandishi Wetu, Songwe

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) wameendelea kufanya mapinduzi makubwa katika kuinua ubora wa elimu nchini, hususan katika masomo ya sayansi. 

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano maalum yaliyosainiwa kati ya pande hizo mbili, yakilenga kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga na kukarabati maabara za sayansi katika shule mbalimbali za mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora.

Halmashauri ya Wilaya ya Ileje mkoani Songwe ni moja kati ya wilaya zilizonufaika na mapinduzi haya ambapo shule mbili zimenufaika na umaliziaji wa ujenzi wa maabara nne za Sayansi. Umaliziaji ujenzi na ukarabati wa maabara hizo unafanyika kwa ufadhili wa Serikali ya Canada, ambapo takribani shilingi milioni 132 zimetumika.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Afisa Miradi kutoka TEA, Bi Atugonza David, alisema shule zilizonufaika ni Shule ya Sekondari Itumba, iliyopokea ruzuku ya shilingi milioni 78.3 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa vyumba viwili vya maabara, na Shule ya Sekondari Bupigu, iliyopokea ruzuku ya shilingi milioni 54 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa maabara mbili za Kemia na Fizikia.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Itumba, Mwl. Didiye Paul, alieleza kuwa ufadhili huo umekuwa wa neema kubwa kwa shule yake ambayo awali haikuwa na maabara hata moja.

“Awali wanafunzi wetu walikuwa wakifanyia mazoezi ya sayansi darasani, jambo lililokuwa likipunguza ufanisi wa ujifunzaji. Kukamilika kwa maabara hizi kumetoa hamasa kubwa na idadi ya wanafunzi wanaojisajili kusoma masomo ya sayansi imeongezeka kwa asilimia 75 kutokana na mazingira kuwa rafiki na ya kuvutia,” alisema Mwl. Paul.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bupigu, Mwl. Shuhudia Mbembela alisema, kilio cha kukosekana kwa maabara ni cha siku nyingi kwa walimu na wanafunzi shuleni hapo hivyo ufadhili walioupata umekuwa mkombozi wao.

“Hadi sasa tumeshakamilisha ukarabati wa maabara moja na nyingine ukarabati unaendelea umefikia asilimia 95,” alisema Mwl. Mbembela.

Mwl. Mbembela aliongeza kuwa kukamilika kwa maabara hizo ni kutimia kwa ndoto ya muda mrefu ya shule hiyo, kwani hapo awali wanafunzi na walimu walikuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo katika mazingira magumu na yasiyo salama.

“Sasa tunaamini ufaulu katika masomo ya sayansi utaongezeka kwa kiwango kikubwa,” alisisitiza.

Kwa ujumla, Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa kushirikiana na UNICEF inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali yenye thamani ya takribani shilingi bilioni 3 katika mikoa ya Songwe, Kigoma na Tabora. 

Miradi hiyo inalenga kuinua ubora wa elimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia, na kupanua fursa za elimu bora na salama kwa kila mtoto wa Kitanzania.

Muonekano wa ndani wa maabara ya sayansi Shule ya Sekondari Itumba zilizokamilishwa na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.
Muonekano wa ndani wa maabara ya sayansi Shule ya Sekondari Itumba zilizokamilishwa na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada
Mkuu wa Shule ya Sekondari Itumba Mw. Didiye Paul (katikati) akiwa pamoja na Afisa miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David wakikagua maabara mbili za sayansi shuleni hapo zilizokamilishwa na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bupigu Mwl. Shuhudia Mbembela akitoa maelezo kwa Afisa miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David, wakati wa ukaguzi wa umaliziaji ujenzi wa maabara mbili za Sayansi shuleni hapo.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bupigu Mw. Shuhudia Mbembela akiwa pamoja na Afisa miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David wakikagua maabara mbili za sayansi shuleni hapo zilizokamilishwa na TEA kwa kushirikiana na UNICEF, kupitia ufadhili wa Serikali ya Canada.
Afisa miradi kutoka TEA Bi. Atugonza David katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu wa Shule ya Sekondari Itumba mara baada ya kukagua ukamilishaji wa ujenzi wa maabara mbili za sayansi shuleni hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...