Dar es Salaam:

Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limezindua matumizi ya Nishati yake safi ya kupikia ya Rafiki Briquettes katika soko la Kimataifa la samaki Feri katika azma ya kupunguza matumizi ya nishati zisizo salaama

Nishati hiyo imepokelewa na watumiaji wakiwemo wachoma samaki, mama na baba lishe wa sokoni hapo wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Matumizi ya Nishati Safi ya Rafiki Briquettes Katika Soko la Kimataifa la Samaki Feri Dar Es Salaam Oktoba 17, 2025.

Akiongea wakati wa hafla hiyo Mhe Edward Mpogolo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala ambaye alimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye hafla hiyo, aliwataka wananchi kuchangamkia fursa za kibiashara kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuwa mawakala wa kusambaza Nishati Safi na salama ya kupikia ya Rafiki Briquettes.

Ameipongeza STAMICO kwa kubuni miradi yenye Ushirika na sekta nyingine nje ya mnyororo wa thamani wa madini inayotunza mazingira na pia kufungua fursa za kibiashara ambazo wananchi wanaweza kuzitumia ili kujiongezea kipato kwa kuuza nishati hii.

Katika mpango huu,ameipongeza STAMICO kwa kushirikiana na taasisi wadau katika kuhakikisha wananchi wanahama kutoka katika matumizi ya nishati safi chafu na kutumia nishati safi

"Tumeona STAMICO imeshirikiana na REA katika kutumia Nishati safi kuchoma nyama kule Arusha, nawakaribisha katika soko la feri ili tuweze kuchoma samaki tunajipanga” alisisitiza Mpogolo

Ametumia fursa hiyo kuwapongeza wanasoko la feri kwa kupokea mabadiliko ya matumizi ya nishati safi bila kuchoka na kuongeza kuwa matumizi ya nishati chafu yana athari kubwa kwa afya za watumiaji na mazingira,hivyo kila mwananchi awe na uelewa wa madhara haya kwa jamii.

Awali, katika hotuba ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mhandisi Baraka Manyama, kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, alisesema kuwa Nishati ya Rafiki Briquettes ni rafiki kwa mazingira,afya ya mtumiaji na rafiki pia kwa bei kulinganisha na nishati nyingine.

“Nishati ya Rafiki Briquettes inatokana na mabaki ya Makaa ya mawe ambayo yamepitia kwenye mchakato wa kiwandani wa kupunguza hewa ya ukaa na ukali wa kuwaka”, amesema.

Ameongeza kuwa Shirika limezindua mpango huu kwa kugawa majiko kumi kwa wakaanga samaki katika soko hilo kama mchango wa STAMICO kuunga mkono agenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya matumizi ya Nishati Safi.

Amedokeza kuwa Shirika kwa sasa linasambaza nishati hii kwa Magereza yote 129 nchini na kwenye taasisi mbalimbali za elimu kama vile shule na vyuo.

Kwa upande wa Soko la Feri, Bwn Selemani Mfinanga ameishukuru STAMICO na Serikali kwa kuendelea kupeleka mabadiliko katika nishati ili kuweza kuendana na kasi ya madadiliko na kwamba wako tayari kushirikiana na kuunga mkono jitihada za kuhamasisha matumizi ya nishati safi.

Kwa upande wa wakala wa STAMICO kutoka Taasisi ya Wanawake na Samia wa Mkoa wa Dar es salaam ambaye ndiye atakayekuwa anasambaza Nishati hii katika soko la feri Bi. Sophia Kinega Ameishukuru STAMICO kwa kuendelea kushirikiana na kuwawezesha kufanya biashara ya Nishati safi katika maeneo mbalimbali jambo linalowavutia Wanawake wengi kushiriki katika jitihada kupunguza matumizi ya nishati zisizo salama kwa kupikia.

Amesema kuwa Shirika limejenga viwanda vikubwa viwili katika Mkoa wa Songwe na Pwani ambavyo vinazalisha nishati hii kwa kiwango kikubwa na kiwanda kidogo kilichopo eneo la TIRDO,Msasani, Dar es Salaam.

STAMICO inaendelea kuongeza viwanda katika maeneo tofauti yakiwemo Mkoa wa Dodoma na Tabora kufikia mwezi Novemba mwaka huu, na baadaye viwanda vingine vikubwa viwili vitakavyofunguliwa katika Mikoa ya Geita na Tanga.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...