Wakulima wa mahindi kutoka Wilaya ya Namtumbo, mkoani Ruvuma, wamepongeza hatua ya serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuanzisha vituo vya ununuzi wa mahindi katika maeneo yao, hatua ambayo wamesema imeleta manufaa makubwa kwao kiuchumi.

Julius Ndemba, mkulima wa mahindi alieuza mahindi kituo cha NFRA Namtumbo, amesema ameweza kuuza mahindi yake kwa bei nzuri kupitia kituo cha NFRA na kulipwa kwa wakati, kinyume na matarajio yake ya awali. 

“Tunaishukuru serikali na NFRA kwa kutusogezea kituo hiki. Tumepata bei ya shilingi 700 kwa kilo moja na fedha zetu tumelipwa kwa wakati."

Kwa upande wake mkulima mdogo Neema Kapinga kutoka Namtumbo, aliishukuru serikali kwa kufungua kituo hicho na kuomba utaratibu wa ununuzi uendelee ili kuwasaidia wakulima zaidi. 

"Watu wengi wananufaika sio tu kwa kuuza mahindi, bali pia kwa kufanya biashara mbalimbali kutokana na wingi wa watu wanaofika katika maeneo haya. Mama lishe na wafanyabiashara wadogo wanapata kipato,” Akitoa wito kwa serikali kuweka mazingira mazuri ya kudumu kwa vituo hivyo.

Afisa Ugavi wa NFRA Kanda ya Songea Tabitha Thomas Mpangala, alisema zoezi la ununuzi linaendelea kwa mafanikio ambapo wakulima wanalipwa kwa awamu kulingana na walivyowasilisha mahindi yao. “Tayari tumelipa fedha kwa wakulima na tunalipa kwa awamu, Tunawapa moyo wakulima waendelee kuleta mahindi yao,” 

Mpangala aliongeza kuwa kwa sasa wakulima wanauelewa mzuri wa ubora wa mahindi yanayohitajika, hali iliyoondoa usumbufu wa awali wa kuchambua mahindi mabovu na mazuri.

Juvenile Fulgence Kapinga kutoka kituo cha ununuzi Namabengo alisema tayari ameweza kuuza mahindi mara tano na ameshapokea malipo yote. “Nimenunua guta la kubebea mahindi ambalo litanisaidia msimu ujao. Pesa zilizobaki nitazitumia kujiandaa kwa kilimo kijacho."

Nao wakulima wengine kama Vestina Athanas Ponela wameeleza namna walivyonufaika na huduma hiyo, Akiwa ameuza mahindi mara nne na kulipwa kwa awamu zote, amesema amepanga kununua pembejeo za kilimo na kuanza ujenzi wa nyumba.

 “Naomba wakulima wenzangu waachane na machinga wanaonunua kwa bei ya hasara ya shilingi 400. Serikali kupitia NFRA inalipa bei nzuri ya shilingi 700 na inawalipa kwa wakati."




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...