Na, Seif Mangwangi, Arusha
Tume huru ya uchaguzi katika Jimbo la Arusha mjini, imewataka wananchi waliopoteza kitambulisho cha mpiga kura kufika kwenye kituo cha kupigia kura na mojawapo ya kitambulisho ikiwemo cha NIDA, hati ya kusafiria au leseni ya udereva na hapo ataruhusiwa kupiga kura.
Wito huo umetolewa leo Oktoba 19, 2025 na msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Arusha Mjini, Shabani Manyama alipokuwa akitoa tangazo la uchaguzi Mkuu 2025 kwa mujibu wa kifungu cha 69(1), cha Sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
“Siku ya uchaguzi ni lazima mpiga kura afike kituoni na kadi yake ya mpiga kura lakini kwa mpiga kura aliyepoteza kadi yake ataruhusiwa kupiga kura endapo atafika katika kituo alichopangiwa akiwa na leseni ya udereva au pasi ya kusafiria au kitambulisho cha Taifa(NIDA),”amesema.
Amesema ikiwa mpiga kura atatumia vitambulisho hivyo majina na kitambulisho mbadala atakachowasilisha yanatakiwa kufanana na yaliyomo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura.
Kwa mujibu wa Tangazo hilo, Manyama amesema uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani utafanyika siku ya Jumatano 29 Oktoba 2025 na kwamba vituo vilivyotumika kuandikishia wapiga kura ndivyo vitatumika kupigia kura.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini humo Manyama amesema kupiga kura ni haki ya kila mtanzania mwenye akili timamu na umri kuanzia miaka 18.
"Vituo vilivyotumika kuandikishia wapiga kura ndivyo vitakavyotumika kupigia kura, vituo vyote vitafunguliwa saa moja kamili asubuhi na kufungwa saa kumi kamili jioni (1:00-10:00), vituo vya kupigia kura vya Magereza vitafunguliwa saa mbili kamili asubuhi na kufungwa saa tisa kamili alasiri (2:00-9:00), “ amesema.
Aidha amesema kila kituo cha kupigia kura kumebandikwa taarifa kama mfano wa karatasi ya kura yenye majina na picha za kila mgombea pamoja na nembo za vyama vyao vya siasa kwa uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Pia amesema taarifa nyingine zilizobandikwa ni orodha ya majina ya wapiga kura walioandikishwa na Tume huru ya taifa ya uchaguzi na orodha ya wapiga kura walioruhusiwa kupiga kura moja tu ya Rais.
Manyama amewataja wananchi wote kupitia taarifa hizo ili kutambua mapema vituo watakavyopigia kura na kuona mfano wa karatasi ya kura.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...