NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

WASHIRIKI zaidi ya 200 kutoka mataifa mbalimbali duniani wamehudhuria Mkutano wa Kwanza wa Dunia wa AI for Climate Action (AICA) unaofanyika nchini Tanzania, ukiwa na lengo la kujenga ujuzi na kuimarisha ushirikiano katika kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kupitia teknolojia ya Akili Bandia (Artificial Intelligence – AI).

Mkutano huo umeandaliwa na Umoja wa Mataifa kupitia Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) uliosainiwa Paris, Ufaransa, na unasisitiza umuhimu wa maendeleo ya teknolojia katika kuboresha ustahimilivu wa mabadiliko ya hali ya hewa na kupunguza uzalishaji wa gesi ukaa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano huo leo, Oktoba 8, 2025 jijini Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Profesa Peter Msoffe, amesema maendeleo ya kasi ya teknolojia duniani yamekuwa kichocheo cha ufanisi katika sekta mbalimbali, hivyo matumizi ya Akili Bandia yatachangia pakubwa katika masuala ya tabianchi, usafi wa mazingira na uhifadhi wa bayoanwai.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliridhia kikao hiki kufanyika hapa Dar es Salaam chini ya usimamizi wa UNFCCC, ili wataalamu wabadilishane uzoefu kuhusu namna Akili Bandia inaweza kutumika kwa ufanisi katika kukabiliana na changamoto za mazingira,” amesema Prof. Msoffe.

Ameongeza kuwa maazimio na mapendekezo yatakayojitokeza katika mkutano huo yatakuwa mwongozo muhimu kwa Tanzania, Afrika na dunia kwa ujumla kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa katika kutatua changamoto za tabianchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mabalozi wa Afrika wanaosimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, Dkt. Richard Muyungi, amesema mkutano huo ni hatua kubwa ya kuimarisha juhudi za bara la Afrika katika kutumia teknolojia mpya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Muyungi amewataka Watanzania, hususan vijana, kutumia fursa ya mkutano huo kujifunza na kujenga uelewa wa kina kuhusu matumizi ya Akili Bandia katika tafiti na mipango ya mazingira, ili kulisaidia taifa kujikinga na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotishia uhai wa viumbe hai.

“Tunapaswa kuwekeza katika maarifa na ubunifu wa kiteknolojia kama nyenzo ya msingi ya kulinda mazingira na maendeleo endelevu,” amesema Dkt. Muyungi.

Miongoni mwa masuala yanayojadiliwa katika mkutano huo ni upatikanaji wa fedha, ujenzi wa uwezo wa kitaalamu, pamoja na matumizi ya teknolojia bunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.



















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...