MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeahirisha kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hadi itakapopangiwa kikao kingine (session).Hatua hiyo imekuja baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Nassoro Katuga kuiomba mahakama ahirishe ili waweze kupata muda wa kujibu mapingamizi yaliyowasilishwa na Lissu akipinga shahidi wa siri kuongea akiwa haonekani.
Mapema, Wakili Katuga alidai mahakamani hapo kuwa leo Novemba 12, 2025 kesi imekuja kwa ajili ya kusikilizwa na wanaye shahidi, lakini shahidi huyo ni mmoja kati ya wale ambao mahakama ilitoa amri ya wao kutoa ushahidi kwa siri.
Hata hivyo, shahidi huyo ambaye alikuwa haonekani alipoitwa mahali alipokuwa amesimama na akaulizwa kama anasikia, ilisikika sauti ndani ya ukumbi wa mahakama kutokea kwenye boksi kubwa la mbao ikisema, “Ndiyo nasikia.”
Lissu alinyoosha mkono mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, akisaidiwa na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, akidai kuwa hakubaliani na shahidi wa siri.
Lissu alitumia hoja saba kupinga utaratibu huo akijikita katika tafsiri za kanuni za ulinzi wa mashahidi, lakini pia akirejea uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu kuhusu ulinzi wa mashahidi katika ombi lililotolewa na Jamhuri mapema wakati kesi hii inaanza juu ya kwamba baadhi ya mashahidi wao watakuwa wa siri.
“Kwa mujibu wa kanuni hizo, kizimba maalum ni eneo ambalo shahidi haonekani na mtu yeyote isipokuwa majaji. Lakini hapa, majaji wenyewe hawawezi kumuona shahidi jambo ambalo halikubaliki kisheria,” alisem Lissu.
“Hicho kiboksi siyo kizimba cha kisheria. Huyo shahidi haonekani hata kwa majaji,” alisema Lissu.
Pia amedai kuwa hakuna sehemu inayoonyesha majina ya mashahidi wanaotakiwa kulindwa yalipelekwa kwa Jaji, kwani ni lazima Jaji aridhike kwamba huyu ni shahidi na maisha yake yako hatarini kweli.
Aidha, alieleza kuwa amri ya ulinzi wa mashahidi iliyotolewa Julai 2025 haikutoa ruhusa ya kutumia kiboksi hicho, na kwamba kanuni mpya za ulinzi wa mashahidi haziwezi kutumika kwa kesi iliyoanza kabla ya kutungwa kwake.
Kwa upande wa Jamhuri, Wakili wa Serikali Mkuu Nassoro Katuga aliomba kuahirishwa kwa shauri hilo ili kupata muda wa kujibu hoja za Lissu, akisema hoja hizo ni nyingi na zinahitaji uchambuzi wa kina.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...