
Wachimbaji wadogo wakiwa na leseni za uchimbaji madini walizopewa wakati wa uzinduzi wa programu hii mwezi Mei,2025.
**
Tarime: Mradi wa Serikali wa kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kutoka vijiji vilivyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime wa kufanya uchimbaji wa kisasa na wenye tija ambao ulizinduliwa mwezi Mei 2025 unaendelea vizuri na maandalizi kwa ajili ya utekelezaji wake kuanza hivi karibuni.
Mradi huu upo chini ya programu ya Serikali ya Mining For a Brighter Tomorrow (MBT) ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2025 hadi 2030 ambayo imelenga kuleta mageuzi katika Sekta ya Madini na imeanzishwa kwa ajili ya kushughulikia changamoto na kuboresha fursa kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili kuongeza ushiriki wa makundi hayo katika mnyororo wa thamani wa madini.
Katika kufanikisha mradi huu unaolenga kuwanufaisha vijana zaidi ya 2000 ,wanawake na wenye ulemavu mgodi wa Barrick North Mara ni mdau mkubwa ambao umetoa leseni zake 13 sambamba na kufadhili mafunzo kwa walengwa ili waweze kuendesha shughuli zao za uchimbaji kwa weledi.
Akihojiwa na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya utekelezaji wa mradi baada ya hatua ya wali ya uzinduzi na Serikali kukabidhi leseni 48 za uchimbaji kwa vikundi vya walengwa, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara, Amini Msuya alisema kwa ushirikiano na Barrick North Mara, tayari mamia ya vijana walengwa wamepatiwa mafunzo ya awali ya kushiriki katika mradi kwa kufanya uchimbaji wa kisasa na wenye tija.

Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara, Amini Msuya.
“Tunaendelea kuwahakikishia wachimbaji wadogo wa madini kutoka vijiji vilivyo jirani na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kuwa mradi huu utakuwa wa mfano kwa Tanzaia na pengine hata kwa Afrika kwa ujumla,kwa kuwa umelenga kuhakikisha makundi mbalimbali katika jamii yanamiliki migodi na kunufaika na biashara ya madini,”alisema Amini Msuya.
Msuya alisema kwa sasa mradi umefikia hatua ya utafiti zaidi na maandalizi ya mpango na bajeti ili kazi ianze kwa mafanikio na ametoa wito kwa walengwa kuendelea kuwa wavumilivu na kuwasiliana na ofisi yake pale wanapokuwa wanahitaji ufafanuzi wa jambo lolote au kutoa mawazo kuhusiana na mradi huo milango ipo wazi.
“Natoa rai kwa wachimbaji wadogo waendelee kuamini serikali pamoja na Mgodi wa Barrick North Mara kwa kuwa ipo dhamira ya kweli ya kuhakikisha wananufaisha na mradi huu”, alisisitiza.

Wakati wa uzinduzi wa mradi huu mwezi Mei,mwaka huu Serikali kupitia Wizara ya Madini ilieleza kuwa hatua hii ni uekelezaji wa Programu ya Mining For a Brighter Tomorrow (MBT) na kuwa mradi huu wa kihistoria na wa kwanza kufanyika nchini baina ya serikali,Mgodi na wananchi wanaozunguka mgodi,umevutia ushiriki mkubwa wa wadau kama Benki ya Dunia(WB) na Baraza la Dhahabu Duniani(WGC) ambao wameonesha dhamira ya kusaidia utekelezaji wake.
Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa hotuba yake ya uzinduzi wa Bunge la 13 amebainisha kuwa katika kpindi kijacho cha miaka mitano Serikali itandelea kutekeleza mipango ya kuwanufaisha Watanzania na taifa kwa ujumla kutoka kwenye sekta ya madini ambayo tayari imeanza kupata mafanikio makubwa katika uchangiaji uchumi wa Taifa.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara,Apolinary Lyambiko wakati wa uzinduzi alisema kampuni imetoa leseni hizo kwa lengo la kuimarisha uhusiano mwema na jamii inayozunguka Mgodi.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...