Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Tume Huru ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma leo Alhamisi Novemba 20, 2025.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Samia amesema tukio la uvunjifu wa amani halikutarajiwa nchini kutokana na historia ya muda mrefu ya utulivu wa kisiasa na usalama ambayo Tanzania imeijenga tangu uhuru.

Rais Samia amesema, Tume hiyo itafanya uchunguzi wa kina kubaini sababu zilizoleta hali hiyo, ikiwemo kutathmini madai ya vijana walioingia barabarani kudai haki zao.

Aidha, amebainisha kuwa serikali inatarajia kujua ni aina gani ya haki ambayo vijana hao walihisi wameikosa.

"Tunatarajia Tume Huru ya Uchunguzi ituangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile. Tunataka kujua ni haki gani vijana walikosa na kwa nini waliamua kuingia barabarani kwa umoja wao kudai haki hiyo," alisema.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametoa wito kwa Tume kuchunguza pia taarifa zinazodai kuwa baadhi ya vijana walilipwa fedha kabla ya kushiriki maandamano, na kubaini chanzo cha fedha hizo pamoja na mchango wa mashirika ya ndani na nje ya nchi katika tukio hilo.

Rais Samia ameendelea kwa kusema kuwa, wakati wa kampeni aliahidi kuunda Tume ya Maridhiano ndani ya siku 100, lakini kutokana na matukio yaliyotokea, ameona ni muhimu kuanza na Tume ya Uchunguzi ili kupata taarifa sahihi zitakazowezesha hatua nyingine kufanyika kwa ufanisi.

"Tume ya Uchunguzi ikimaliza kazi na kutuletea mapendekezo, ndipo tutajielekeza kwenye utekelezaji wake kupitia Tume ya Maridhiano kwa lengo la kuimarisha umoja na kuondoa changamoto za kisiasa," alisema.

Kwa ujumla, hatua ya kuanzishwa kwa Tume hii inaonekana kuwa sehemu ya mwelekeo mpana wa Serikali katika kuendelea kuimarisha misingi ya uwazi na utawala bora.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...