NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Tanzania inaendelea kukabiliwa na ongezeko la uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele na mitetemo, hali inayosababishwa na kuongezeka kwa makazi ya watu pamoja na shughuli za biashara na viwanda katika maeneo mbalimbali.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uzingatiaji wa Sheria Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Hamadi Taimuru amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na tatizo hilo kwa kusimamia kikamilifu Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 pamoja na kanuni zake.

Amesema sheria hiyo ndiyo msingi mkuu wa udhibiti wa kelele nchini, huku NEMC likipewa jukumu la kufuatilia viwango vya kelele, kutekeleza masharti ya kanuni, na kuhakikisha kuwa taasisi, biashara na wananchi wanazingatia matakwa ya mazingira.

“Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Viwango vya Udhibiti wa Kelele na Mitetemo) za mwaka 2015 zinaeleza wazi kuwa ni marufuku mtu yeyote kutoa kelele kupita kiasi au zisizo za lazima. Kanuni zimeainisha viwango maalumu vya kelele kulingana na aina ya maeneo kama makazi, biashara, viwanda na taasisi nyeti kama hospitali na shule,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa tafiti zinaonyesha madhara makubwa ya kiafya yanayotokana na kukaa kwenye maeneo yenye kelele kupita kiasi, ikiwemo kupungua kwa usikivu, msongo wa mawazo, uchovu, shinikizo la damu, matatizo ya moyo na usingizi usio na utulivu. Kwa watoto, kelele husababisha kupungua kwa umakini na kuathiri uwezo wa kujifunza, hali inayodumaza maendeleo yao.

Hata hivyo, amesema bado zipo changamoto katika utekelezaji wa udhibiti wa kelele na mitetemo, ikiwemo ushirikiano mdogo kati ya taasisi zinazohusika na uhaba wa vifaa na rasilimali katika mamlaka za serikali za mitaa, jambo linalochelewesha ufuatiliaji wa viwango vya kelele katika maeneo mbalimbali.

Amesisitiza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano wa wadau na kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha wananchi wanaishi katika mazingira tulivu na salama.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...