NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimesaini mikataba na makampuni mbalimbali kwa ajili ya ufungaji wa samani na miundombinu ya TEHAMA kwenye majengo 21 mapya chini ya Mradi wa Mageuzi ya Kiuchumi katika Elimu ya Juu (HEET).

Akizungumza katika hafla hiyo leo Novemba 28, 2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Balozi Mwanaidi Sinare Maajar, amesema Baraza linaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo muhimu unaotarajiwa kuongeza tija katika maeneo ya taaluma, utafiti na utoaji huduma kwa umma.

“Baraza limehakikisha kupitia vyombo vyake mbalimbali kuwa mradi unatekelezwa kwa weledi na uadilifu ili kufikia malengo ya Chuo. Tunasisitiza kila mhusika atimize wajibu wake kwa ufanisi na kwa wakati unaotakiwa,” amesema Balozi Maajar.

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Bernadeta Killian, amesema utekelezaji wa shughuli za TEHAMA chini ya HEET umefikia asilimia 70, kiwango ambacho ni sawa na asilimia 60 ya malengo ya Mpango wa Kampasi Janja.

Amefafanua kuwa hatua ya msingi ilikuwa kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, ambapo kwa sasa Chuo kina mtandao mpya wa msingi (core network) wenye ufanisi zaidi, usalama wa kutosha na mfumo wa umeme wa dharura unaowezesha upatikanaji wa huduma muda wote.

Prof. Killian amesema uwekezaji huo umeongeza kasi ya usambazaji mtandao kutoka 1.5Gbps hadi 10Gbps, hatua inayowezesha mabweni, maktaba na vitengo mbalimbali kunufaika na huduma za kidijitali kwa kiwango cha juu.

“Mikataba iliyosainiwa leo ndiyo itakayokamilisha miundombinu ya kufikisha mtandao katika vitengo mbalimbali na kuwezesha matumizi ya kasi mpya ya 10Gbps,” amesema.

Ameongeza kuwa UDSM imejenga kituo kipya cha data (data center) chenye uwezo mkubwa wa kuendesha mifumo yote ya kitaasisi, ikiwemo mifumo ya kujifunzia na kufundishia, rasilimali watu, usimamizi wa taarifa za wanafunzi, barua pepe na mifumo mingine ya kiutumishi.

Kwa sasa, jumla ya wafanyakazi 2,684 wanatumia mfumo wa barua pepe ulioboreshwa, huku uwezo wa kila akaunti ukiongezeka kutoka 500MB hadi 5GB.

Aidha, amesema uwekezaji wa HEET umeweka msingi wa kuwa na Chuo chenye miundombinu ya kisasa, mifumo ya utawala ya kidijitali, mazingira jumuishi ya kujifunzia na mifumo ya uzalishaji maarifa inayoendana na mahitaji ya karne ya sasa.


















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...