NA EMMANUEL MBATILO, DODOMA

Taasisi ya HakiElimu Tanzania imefanya mafunzo kwa wadau wake ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa SAUTI ZETU ambao umejikita katika kusisitiza ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika mambo mbalimbali ya kijamii.

Mafunzo hayo yametolewa kwa wafanyakazi wa mashirika yanayosimamia mradi huo yakiwemo Child Support Tanzania (CST), Sawa Wanawake Tanzania (SAWA), Organization for Community Development (OCODE), Mtwara non- governmental organization network (MTWANGONET), Save Education and Future Development Trust pamoja na viongozi wa jamii wakiwemo Walimu Wakuu, Watendaji kutoka serikali za mitaa, Maafisa Elimu kutoka Wilaya za Bagamoyo, Mtwara, Ifakara, Mbeya Jiji pamoja na Mvomero.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo 
Novemba 20, 2025 Jijini Dodoma, Mtaalamu wa Jinsia na Maendeleo wa HakiElimu, Bi. Nuria Mshare, amesema lengo kuu ni kuwawezesha wadau kutekeleza shughuli za maendeleo kwa kuzingatia usawa wa kijinsia na kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.

“Tunatarajia kuona taasisi zinatoa kipaumbele kwa makundi ambayo mara nyingi yamesahaulika, ikiwemo watu wenye ulemavu, wanawake, wasichana na jamii za pembezoni, katika kupanga na kutekeleza bajeti zao,” amesema Bi. Nuria.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Miradi na Uchechemuzi wa CST mkoani Mbeya, Dkt. Hildergade Mehrab, amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi yote inawajumuisha wananchi wote bila ubaguzi.

“Ni muhimu kumpa nafasi mnufaika wa mwisho kushiriki kuanzia hatua ya kuunda mradi hadi tathmini yake. Hii inasaidia kupata maoni ya pande zote—wananchi, wataalamu na serikali,” amesema Dkt. Mehrab.

Naye Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika la Sawa Wanawake Tanzania (SAWA), Bi. Leonora Ngowi, amesema mafunzo hayo yameonesha umuhimu wa kushirikisha jamii katika elimu ya mtoto ili kujenga mazingira rafiki ya kujifunza.

“Jamii ikishiriki kikamilifu, watoto hupata msaada wa kutosha na mazingira bora ya elimu, kwani kila upande unatambua wajibu wake,” amesema.

Kwa upande wa walimu, Bw. Jangson Mwang’ombola, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Lusanga kutoka Mvomero, amesema mafunzo hayo yamempa motisha kuhamasisha elimu jumuishi katika jamii.

“Elimu jumuishi inaweka pamoja watoto wenye changamoto na wasiokuwa nazo, na wote hupata nafasi sawa ya kujifunza bila kuangalia ulemavu,” amesema Mwang’ombola.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nianinjema kutoka Bagamoyo, Bw. Renatus Kisenha, ameongeza kuwa mafunzo hayo yametoa uelewa zaidi kuhusu namna ya kuondoa unyanyapaa na kuimarisha ushirikiano kati ya walimu, wazazi na wanafunzi.

HakiElimu imesisitiza kuwa itaendelea kufanya mafunzo kwa wadau mbalimbali nchini ili kuhakikisha misingi ya usawa, ujumuishaji na ulinzi wa haki za mtoto vinazingatiwa katika elimu na maendeleo ya jamii. 






























Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...