Na Saidi Lufune, Dodoma
WIZARA ya Maliasili na Utalii inaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya misitu na ufugaji nyuki ili kuboresha uhifadhi na uendelezaji wa rasilimali za misitu na nyuki, pamoja na kukabiliana na changamoto zinazokabili sekta hizi. Lengo ni kuhakikisha faida za sekta hizi zinanufaisha jamii na taifa kwa ujumla.

Hayo yalielezwa jijini Dodoma na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki wa Wizara hiyo, Bw. Daniel C. Pancras, wakati wa ufunguzi wa warsha iliyowakutanisha wataalamu na wadau wa sekta ya misitu na nyuki. Warsha hiyo ililenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu mikakati ya kuendeleza sekta hizi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali za misitu na nyuki.

“Sekta ya misitu na nyuki imekuwa na mchango mkubwa katika ongezeko la ajira kwa vijana na wanawake, na pia imechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa. Hata hivyo, sekta hii inakabiliwa na changamoto kadhaa, na kupitia warsha hii, tunapanga mikakati ya pamoja ya kutatua changamoto hizo,” alisema Bw. Pancras.

Akiendelea, Pancras alisisitiza kuwa mikakati inayopendekezwa katika warsha hii inapaswa kutoa matokeo chanya na ya haraka katika utekelezaji wa sera na malengo ya Wizara, huku ikizingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Hii ni pamoja na kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya misitu na asali, na kuhakikisha sekta ya misitu inapata maendeleo endelevu.

Katika hatua nyingine, Pancras alitoa wito kwa wadau wa sekta ya uhifadhi na utalii kushiriki kikamilifu katika kuwania Tuzo za Uhifadhi na Utalii, maarufu kama The Serengeti Awards. Tuzo hizi zinatolewa kwa kutambua michango ya wadau katika kuendeleza sekta ya maliasili na utalii nchini. Alisisitiza umuhimu wa wadau kuwa mabalozi wazuri kwa kuhamasisha wengine kuhusu uwepo wa tuzo hizi.

Wadau walioshiriki warsha hiyo ni pamoja na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF), vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania Beekeepers Development Organization (TABEDO), wawakilishi kutoka Ofisi za Wakuu wa Mikoa ya Dodoma na Morogoro, Shirika la Nyumba la Taifa, na Bodi ya Wandalasi.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...