Na Oscar Assenga, LUSHOTO.
JESHI la Polisi Mkoa wa Tanga linamshikilia Mkazi wa Welei wilayani Lushoto mkoani Tanga Isaka Clement Ngulizi kwa kosa la kumshambulia na kumkata vidole vitatu mwanafunzi wa darasa la nne mwenye umri wa miaka kumi na moja (11).
Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Muchunguzi alisema kwamba tukio hilo lilitokea Desemba 2 mwaka huu ambapo mtuhumiwa huyo alitekeleza ukatili huo kwa kisingizio cha kumkuta mtoto huyo akijaribu kuiba ndani ya nyumba yake.
Alisema kutokana na mazingira ya matukio hayo Jeshi hilo linatoa wito kwa jamii hususani wazazi na walezi kuongeza umakini na ulinzi kwa watoto wadogo hususani katika kipindi cha sikukuu.
Aidha alisema kwamba katika kipindi hicho mara nyingi hutawaliwa na baadhi ya wazazi na walezi kuwaacha watoto kwenda kutembea peke yao bila uangalizi wa mtu mzima kwenye akili timamu.
“Jeshi la Polisi linatoa onyo kali kuwa kujichukulia sheria mkononi ni kosa la jinai na hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika mbele ya sheria kwa kumfanyia mtu mwengine ukatili”Alisema.
Kamanda Muchunguzi alisema Jeshi hilo limepata mafanikio makubwa katika kushughulikia matukio ya ukatili dhidi ya watoto mkoani hapa.
Alisema kwamba katika tukio la kwanza ambalo lilitokea Octoba 8 mwaka huu katika Kijiji cha Kiloza wilayani Korogwe ambapo mmoja wa mtoto mwenye umri wa miaka mitatu(03) alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa mguu wa kulia na kitu chenye makali.
Alimtaja mtuhumiwa aliyemjeruhi vibaya ni Abraham Yonathani Shelutete huku akieleza kwamba uchunguzi ulibainika kuwa mtuhumiwa alifanya ukatili huo kutokana na wivu wa mapenzi.
Alieleza kwamba kufuatia ushahidi uliokusanywa na kuwasilishwa mahakamani Novemba 19 mwaka huu mtuhumiwa alipatikana na hatia ikiwemo kuhukumiwa kifungo cha miaka (07) Gerezani pamoja na amri ya kulipa fidia ya Sh.100, 000 kwa madhara.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...