NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Benki ya Standard Chartered Tanzania imetoa elimu ya fedha kwa wanafunzi zaidi ya 120 pamoja na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTU), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha vijana kwa ujuzi wa kifedha na kitaaluma.

Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kukuza uelewa wa masuala ya kifedha nchini, sambamba na malengo ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya kuimarisha uraia wa kifedha unaochochea maendeleo ya wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo Desemba 12, 2025 Jijini Dar es Salaam, Meneja wa Uzingatiaji Sheria wa Standard Chartered Tanzania, Ilago Mabelya, amesema mafunzo yalilenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutunza fedha, kukopa kwa uwajibikaji na kuwekeza kwa busara.

Amesema changamoto kubwa kwa vijana wengi ni kushindwa kutofautisha mahitaji na matakwa, hali inayosababisha matumizi yasiyo na tija.

“Ni muhimu vijana kujifunza kupanga vipaumbele vya matumizi, wakizingatia zaidi mahitaji muhimu kuliko matakwa,” amesema Mabelya.

Ameongeza kuwa wanafunzi wanaopanga kuwekeza wanapaswa kuzingatia faida za muda mrefu na akasisitiza umuhimu wa kuwekeza katika hisa na hatifungani kama njia ya kuongeza kipato na kujiandaa kwa maisha ya baadaye, ikiwemo kipindi cha kustaafu.

Akifungua rasmi mafunzo hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini upande wa Usimamizi wa Rasilimali na Utawala, Profesa Sylvia Temu, ameishukuru Standard Chartered Tanzania kwa kushirikiana na chuo hicho katika kutoa elimu ya kifedha kwa wanafunzi.

Profesa Temu amesema elimu ya fedha huwajengea watu maarifa, ujuzi na tabia ya uwajibikaji katika usimamizi wa fedha zao, akibainisha kuwa wanafunzi hupata fedha kutoka vyanzo tofauti ikiwemo mikopo na misaada ya ndugu.

“Ni muhimu wanafunzi kujua namna ya kugawa fedha zao kwa kodi, mahitaji ya kila siku, akiba na uwekezaji,” amesema.

Amewahimiza wanafunzi kuweka akiba ya angalau asilimia 20 ya mapato yao ili kujenga msingi wa nidhamu na uwajibikaji wa kifedha.

Kwa upande wake, mhadhiri wa Saikolojia wa chuo hicho, Dkt. Hyasinta Kessy, amewahimiza wanafunzi kuepuka matumizi ya anasa na kuelekeza nguvu zao katika uwekezaji wa mali zinazodumu kama viwanja na vifaa muhimu vya nyumbani.

Naye Mkuu wa Shule ya Biashara ya chuo hicho, Dkt. Abdul Abayo, amesisitiza umuhimu wa kuanza kuokoa hata kiasi kidogo cha fedha, akisema akiba ndogo inaweza kuwa msaada mkubwa wakati wa changamoto za kifedha.

Baadhi ya wanafunzi wameeleza changamoto ya kukosa mitaji ya kuanzisha uwekezaji, ambapo walipewa elimu kuwa hata akiba ndogo, ikiwa itawekwa kwa nidhamu kupitia taasisi za kifedha, inaweza kukua na kuwa rasilimali muhimu baadaye.

Mafunzo hayo yameendeshwa na Financial Education Champions wa Standard Chartered waliohitimu mafunzo maalumu ya Benki Kuu ya Tanzania, na yaliwapa washiriki fursa ya kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu usimamizi bora wa fedha, huku wengi wakionesha kuridhika na kupongeza mpango huo.















Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...