NA VICTOR MASANGU,KIBAHA
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, Dr. Catherine amekemea tabia ya baadhi ya watumishi kushindwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuagiza kuimarishwa kwa huduma za wateja katika vituo vya afya ili kuboresha huduma ya matibabu.
Pia ametoa wito kwa kamati za afya kuhakikisha wanaweka misingi mizuri ya kujadili kwa kina taarifa za takwimu zilizowasilishwa katika kikao cha tathmini ya mwaka 2024/2025 kwa Divisheni ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe.
Hayo ameyabainisha wakati wa kikao hicho cha tatmini kwa kipindi cha mwaka wa 2024/2025 Dkt. ambapo amebainisha kuwa idara ya afya wanapaswa kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa kiwango cha asilimia 50 hadi kufikia kipindi cha tathmini.
Kadhalika amesisitiza kuna umuhimu mkubwa wa kuweka mikakati madhubuti ya upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi wote, wakianza na kaya zenye mahitaji maalum.
Amesema kuwa mpango wa bima ya afya kwa wote utaanza kwa kaya ambazo zitachangia kiasi cha shilingi 150,000 kwa mwaka kwa ajili ya baba, mama na watoto, na kuagiza utolewaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kujiunga na mpango huo.
Aidha, ameongeza kuwa kuanzia Januari 2026, kituo cha afya cha Kilimahewa kianze kutoa huduma rasmi. Alionya kuwa mtu yeyote aliyepokea fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi lakini hawezi kuumaliza, anatakiwa kutoa taarifa mapema kwa uongozi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Kitengo cha Dharura, Dkt. Majaliwa, alieleza kuwa kuna upungufu mkubwa wa wauguzi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Pwani, na kueleza kuwa walipo ni wachache na hawapati posho zao kwa wakati.
Pia amebainisha kuwa madereva wa sekta ya afya pia hukumbwa na changamoto hiyo hiyo ya kucheleweshwa kwa malipo yao.
Naye mwakilishi kutoka Ofisi ya Utumishi wa Umma Happyness Anania akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha amewataka watumishi kuhakikisha changamoto zinazowakabili zinafikishwa kwa viongozi wao moja kwa moja.
Ameingeza kuwa lengo kubwa ni kuhakikisha watumishi wanasililizwa kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi wa kina na kusisitiza suala la umuhimu wa kubuni njia mpya za kuongeza mapato kupitia sekta ya afya.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...