Na Pamela Mollel,Arusha

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimefungua Kesi Na. 56/2025 katika Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki kikilalamikia hatua ya Serikali ya Tanzania kuzima mtandao kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, 2025.

Kwa mujibu wa mawakili wanaoiwakilisha LHRC, Wakili Peter Majanjara na Wakili Jebra Kambole, kuzimwa kwa mtandao kulitokea ghafla majira ya saa tano asubuhi Oktoba 29 na kuathiri huduma zote za mawasiliano nchini kwa siku saba mfululizo.

LHRC imedai kuwa hatua hiyo iliathiri Watanzania kiuchumi na kijamii, ikiwemo kukwama kwa miamala ya benki mtandaoni, huduma za afya za kimtandao, pamoja na kupotea kwa fursa muhimu za kupata taarifa katika kipindi cha uchaguzi. Kituo kimesema kitendo hicho kilisababisha hasara ya mamilioni ya shilingi.

Serikali ilieleza kuwa kuzima mtandao kulikuwa kwa madhumuni ya kuzuia vurugu, lakini LHRC inadai sababu hiyo haikidhi misingi ya demokrasia, haikuwa ya kisheria, wala ya lazima.

Kituo hicho kinaomba mahakama itamke kuwa hatua hiyo ilikiuka vifungu 6(d), 7(2) na 8(1)(c) vya Mkataba wa EAC wa mwaka 1999, na kutoa amri inayozuia Serikali kurudia kuzima mtandao bila sheria au amri ya mahakama.

Inatarajiwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania atajibu maombi hayo ndani ya siku 45 baada ya kupokea ilani kutoka kwa Msajili wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...