Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wamesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia 3 Desemba 2025 hadi 2 Desemba 2030. Kusainiwa kwa makubaliano haya ni ishara thabiti ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano uliodumu kwa muda mrefu baina ya taasisi hizo mbili na wadau wengine wenye maslahi mapana kwa taifa.
Licha ya kusainiwa, ushirikiano kati ya NBAA na BoT si jambo jipya, kwani taasisi hizi zimekuwa zikishirikiana kwa miaka mingi katika kuwaelimisha na kuwahabarisha wahasibu, wakaguzi wa hesabu, wataalamu wa kodi, wataalamu wa masuala ya fedha na benki, pamoja na wadau wengine kuhusu masuala mbalimbali yanayogusa maendeleo ya uchumi wa taifa. Makubaliano haya mapya yanakwenda kuongeza nguvu zaidi za kiutendaji na kuratibu kwa ukaribu juhudi za pamoja katika masuala ya kitaaluma na kitaasisi.
Katika dunia inayoendelea kukabiliwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na masuala ya uendelevu (sustainability), makubaliano haya yamelenga pia kuhakikisha kuwa ajenda ya uendelevu inapata nafasi ya msingi katika mipango na utekelezaji wa shughuli za taasisi hizo, kwa lengo la kuandaa kesho iliyo bora kwa vizazi vijavyo.
Makubaliano hayo yamesainiwa rasmi na Gavana wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, ambapo pande zote mbili zimekubaliana kuwa makubaliano hayo yanaweza kuongezewa muda pindi yatakapofikia ukomo wake. Hatua hii imeelezwa kuwa ni mfano mzuri wa ushirikiano endelevu unaopaswa kuigwa na taasisi nyingine nchini, huku mlango ukifunguliwa kwa wadau wengine kujumuika katika juhudi za pamoja za kujenga Tanzania yenye misingi imara ya kiuchumi na kitaasisi.
Hati hiyo ya makubaliano imesainiwa katika Warsha ya Kila Mwaka ya Wahasibu (Accountants Annual Conference) inayofanyika katika APC Hotel and Conference Centre, Bunju – Dar es Salaam, warsha ambayo imeanza 3 Desemba 2025 na inatarajiwa kumalizika tarehe 5 Desemba 2025 kwa washiriki kutembelea vivutio vya utalii katika misitu ya Pugu–Kazimzumbwi, pamoja na kushiriki zoezi la kupanda miti kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za kulinda mazingira.
Kupitia makubaliano haya, taasisi hizo mbili pia zimekubaliana kubadilishana taarifa mbalimbali za kikodi na kihesabu, sambamba na kuoanisha mifumo yao kwa lengo la kuongeza ufanisi. Hatua hiyo imechagizwa zaidi na uzinduzi wa mfumo mpya wa NBAA ujulikanao kama NBAAVN, ambao utawezesha wadau kupata taarifa sahihi za hesabu na kuondoa kabisa uwezekano wa kutumiwa kwa taarifa bandia, kwani sasa kila taarifa ya hesabu itatambulishwa kwa namba maalumu.
Hii ni hati ya tatu ya makubaliano kusainiwa na NBAA mwaka huu 2025, baada ya kusaini makubaliano na Taasisi ya Wahasibu, Wakaguzi na Washauri wa Kodi Zanzibar (ZIAAT) tarehe 16 Mei 2025, na makubaliano mengine na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tarehe 16 Julai 2025, hatua zinazoonyesha dhamira ya NBAA ya kuimarisha mahusiano na kufanya kazi kwa karibu na taasisi muhimu nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania(NBAA), CPA Pius A. Maneno pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba wakisaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitano wakati wa mkutano mkuu wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania(NBAA), CPA Pius A. Maneno pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba wakionesha hati ya makubaliano ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitano mara baada ya kusaini hati hiyo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania(NBAA), CPA Pius A. Maneno pamoja na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba wakibadirishana hati ya makubaliano ya ushirikiano kwa kipindi cha miaka mitano mara baada ya kusaini hati hizo wakati wa mkutano mkuu wa mwaka 2025.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka 2025 wa wahasibu na wakaguzi wa hesabu ulioandaliwa na Bodi ya Taifa ya Uhasibu na Ukaguzi wa Hesabu (NBAA) kufanyika katika hoteli ya APC Bunju jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia S. Temu akizungumza kuhusu mikakati mbalimbali ya kusimamia Taaluma ya Uhasibu na Ukaguzi wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mwaka 2025.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania(NBAA), CPA Pius A. Maneno akielezea maendeleo mbalimbali yanayoletwa na Taaluma ya Uhasibu


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...