Na Mwandishi Wetu, WMTH-Dodoma

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), tarehe 15 Disemba 2025 amefanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya ziara za kutembelea taasisi zilizo chini ya Wizara yake.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhe. Waziri Kairuki ameipongeza Menejimenti na watumishi wa Tume hiyo kwa mafanikio yaliyopatikana ndani ya muda mfupi tangu kuanzishwa kwake, hususan katika utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi. Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio hayo yasije yakasababisha kubweteka, bali yawe chachu ya kuendelea kuzingatia misingi na malengo ya kuanzishwa kwa sheria hiyo.

Waziri Kairuki ameeleza kuwa lengo kuu la Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ni kulinda taarifa binafsi za wananchi, ikiwemo namna taarifa hizo zinavyokusanywa, kuchakatwa na kuhifadhiwa, pamoja na kuhakikisha wakusanyaji na wachakataji wa taarifa wanazingatia taratibu za usajili, uwajibikaji na haki za wamiliki wa taarifa.

Aidha, amekumbusha kuhusu maelekezo ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yaliyotolewa mwaka 2024, na kuitaka Tume kuyatekeleza kikamilifu maelekezo hayo, hususan yale ambayo bado hayajafanyiwa kazi kwa ukamilifu.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma ili wananchi waweze kufahamu uwepo wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, masharti na matakwa yake, pamoja na dhana nzima ya ulinzi wa taarifa binafsi. Amesema elimu hiyo itawawezesha wakusanyaji na wachakataji wa taarifa kuelewa taratibu za usajili, wajibu wa kuwasilisha taarifa za mara kwa mara na namna ya kuzingatia matakwa ya sheria.

“Tuendelee kupambana kwa nguvu zote katika kutoa elimu kwa umma, kwani ni jambo la msingi sana. Mmefanya kazi kubwa ndani ya muda mfupi na kufikia idadi nzuri ya waliosajiliwa, lakini bado wapo wengi ambao hawajafikiwa. Mna jukumu kubwa la kuwafikia ili nao waweze kuwajibika na kutii sheria,” amesema Waziri Kairuki.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...